Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS DKT. MWINYI AFUNGUA KONGAMANO LA SITA LA USAFIRI WA ANGA LA AFRIKA MASHARIKI

Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kwa kushirikiana na Wakala wa Uangalizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Afrika Mashariki  (EAC CASSOA)  imeandaa Kongamano la Sita la Usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kongamano hilo linafanyika katika Hoteli ya Verde, Zanzibar kuanzia tarehe 15 hadi 16 Mei, 2024. 

Kongamano hilo limefunguliwa na Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi .

Dkt. Mwinyi alitoa wito kwa Mamlaka EAC-CASSOA kuanzisha kanuni za pamoja za usalama wa anga ambazo zitasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo kwa sasa. Ameeelezea kuwa Tanzania inachukua hatua na itaendelea kufanya maboresho mengi kwenye usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kujenga viwanja vipya vya ndege pamoja na kuboresha viwanja vilivyopo  ili kuwa na hadhi inayostahili na kutoa huduma nzuri kwa wasafiri.

Aidha, wakati wa ufunguzi viongozi wengine walielezea changamoto mbalimbali zinazokabili usafiri wa anga katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za usafiri ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kitokuwepo kwa kanuni za pamoja na ukosefu wa fedha ili kufanya maboresho yanayohitajika katika sekta hiyo. 

Akiongea kwenye Kongamano hilo Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Joseph Ntakirutimana amezungumzia suala la uwepo wa gharama kubwa za kusafiri kwa ndege ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki akitolea mfano, gharama za tiketi kutoka Kinshasa, DR Kongo hadi Arusha, Tanzania ambayo ni kubwa kuliko gharama kutoka Tanzania kwenda Marekani na kwingineko duniani. Hivyo, ametolea wito kwa Serikali kuungana na kuona namna wanavyoweza kutatua changamoto hizo kwa pamoja. 

Kongamano hilo litajadili baadhi ya masuala ikiwemo usafiri wa anga na namna ya kujenga imani na usalama kwa watumiaji; kuongeza ufahamu wa fursa na ubunifu katika usafiri wa Anga; Masuala endelevu ya kuimarisha Usafiri wa Anga; na Kubadilishana uzoefu, taarifa na maarifa kuhusu usalama wa Usafiri wa Anga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.   

Kongamano hilo limehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Wakili Stephen Byabato, Mawaziri kutoka nchi za Afrika Mashariki, Wakurugenzi Wakuu wa Mamlaka za Usafiri wa Anga na wadau wengine muhimu litawakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya usafiri wa anga wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili kwa pamoja masuala yanayohusu usalama wa usafiri wa anga na Mazingira katika Kanda ya Afrika Mashariki. 

Mada kuu ya Kongamano hilo ni   "Mustakabali wa Usafiri wa Anga - Kudumisha mifumo ya Usafiri wa Anga thabiti, endelevu, yenye ubunifu na salama”. (The future of Aviation – Maintaining resilient, sustainable, innovative, safe, and secure aviation systems).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com