Na Deogratius Temba; Chamwino
WANAWAKE wametakiwa kujiimarisha kiuchumi kwa kuwekeza kwenye miradi mikubwa na kushiriki kwenye nafasi za uongozi na maamuzi katika ngazi mbalimbali ili kubadili mfumo itakayoweka mazingira wezeshi kwa wanawake kufanya biashara.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza, wakati wa kufunga mafunzo ya wanawake viongozi yanayolenga kuongeza kasi ya kuwezesha wanawake vijiji ni, na kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi wa serikali za Mitaa mwaka huu 2024, yanayofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino , Mkoani Dodoma.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa kuongeza kasi ya uwezeshaji wanawake vijijini, unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (Unwomen) unaotekelezwa katika wilaya ya Chamwino.
“wilaya ina kata 36, madiwani wanaume ni 35 na mwanamke Diwani wa kata ni mmoja pekee, vijiji 107 lakini mwanamke mwenyekiti ni mmoja pekee. Hii sio sawa, hakuna usawa wa Kijinsia katika uongozi, tunahitaji mabadiliko makubwa katika eneo hili. Tuongeze wanawake viongozi tafadhali” ,alisema Mwajuma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TWCC, Mercy Silla, alisema kwamba, wanawake wanatakiwa kumiliki uchumu wa viwanda vikubwa na miradi mingine mikubwa ili kujikwamua kiuchumi, kubadilisha kaya zao kiuchumi na kujiwezesha kiuchumi ili waweze kugombea nafasi za uongozi.
“Tunataka wanawake wamiliki miradi mikubwa yenye fedha. Kugombea uongozi unahitaji fedha na unahitaji kuwa vizuri kiuchumi, familia za viongozi ni lazima ziwe na ustawi, ndio maana TWCC tunasisitiza, wanawake wafanyabiasha kuboresha biashara zao, na kuhakikisha wanajitokeza kugombea nafasi za uongozi sambamba na kuingia kwenye nafasi za maamuzi ili wakabadilishe sera ambazo haziwapi nafasi wanawake kuwa wawekezaji au wafanyabsiahara wakubwa”,alisema Sila.
Lakini pia amesema kwamba, wanawake watakapokuwa kwenye uongozi watapata nafasi ya kutoa elimu na kubadilisha mitazamo hasi, mila na desturi kandamizi zilizoko kwenye jamii juu ya uwezo wa wanawake viongozi.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Deogratius Temba, ambaye ni mtaalam na mkufunzi wa masuala ya Jinsia na uongozi, na kuwajumuisha viongozi wanawake kutoka katika ngazi ya Kitongoji, ujumbe wa serikali za Mitaa, kamati na bodi mbalimbali na madiwani wanawake kutka kata 18 za mradi huo.
Social Plugin