Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) utaanzisha kituo cha taarifa na maarifa Kata ya Lembeni Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro ambacho ni kitovu cha harakati ngazi ya kata kwa ajili ya kufuatilia changamoto zilizoibuliwa na wananchi kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi.
Mwezeshaji wa mafunzo kutoka TGNP, Schola Makwaia amesema Kituo cha taarifa na maarifa kitaundwa na wananchi waliopatiwa mafunzo ya uraghibishi kwa siku tano ambayo yalitoa fursa ya wananchi kufanya utambuzi, uchambuzi na kisha utatuzi wa changamoto hizo kwa kushirikiana na viongozi wao.
“Baada ya wananchi kupewa mafunzo ya leo wamekutana na viongozi wao ngazi ya Kata, wakiwemo Mtendani wa Kata, Polisi Kata, Dawati la jinsia, afisa elimu Kata na Afisa Ugani, ambapo Wamekubali uwepo wa changamoto hizo na kukubaliana namna bora ya kushirikiana katika kuzitatua” Amesema Schola
Kwa upande wa viongozi wa kata walioshiriki mafunzo hayo wamesema ili kutokomeza changamoto zilizoibuliwa na wananchi ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia, mfumo dume, pamoja na huduma za kijamii elimu inahitajika zaidi kwa wananchi pamoja na ushirikiano katika ufuatiliaji wa matukio hayo.
Iren Kilembe ambaye ni Mtendaji wa kata ya Lembeni, anapongeza hatua ya kutoa mafunzo iliyofanywa na Mtandao wa TGNP na uahidi kushirikiana na wananchi kwenye kamati za mtakua ambazo pia zinahusika katika kupinga ukatili wa wanawake na Watoto, na kutoa elimu hiyo katika jamii.
Kwa upande wa Changamoto zinazokabili wanawake kwenye masuala ya uongozi Grace Elisha ambaye ni Mshiriki amdsema kupitia mafunzo hayo ameweza kujua sababu ya wanawake kuendelea kuwa nyumba kwenye kugombea uongozi, ikiwemo mfumo dume pamoja na mila na desturi kandamizi ambazo jamii inatakiwa kupewa elimu kuondokana na mila hizo.
“Nikiwa kama Polisi Kata wa Kata hii ya Lembeni naipongeza TGNP kwa kuwa wadau muhimu kuhakikisha ukatika wa kijinsia unatokomezwa na wananchi wanapata elimu namna ya kukabiliana na matukio hayo na kupitia mafunzo haya tumekuwa na uelewa mpana katika kukabiliana na matukio hayo” John Marimu Polisi Kata ya Lembeni
Katika mafunzo hayo ya uraghibishi washiriki waliweza kupitia maeneo manne ikiwemo Changamoto zinazokwamisha wanawake kuwa viongozi, hali ya ukatili wa kijinsia na kingono, mabadiliko ya tabia nchi, kilimo hai pamoja na na hali ya huduma za kijamii.