Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji eneo la Kwembe kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Kata za Kwembe, Msigani na King'azi.
Utekelezaji wa mradi huo ni muendelezo wa mpango maalumu wa kuboresha huduma ya majisafi katika maeneo hayo ikiwa ni agizo la Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso kwa DAWASA kuhakikisha huduma ya maji katika maeneo hayo inaboreshwa.
Msimamizi wa mradi, Mhandisi Jackson Richard amesema utekelezaji wa mradi wa maji Kwembe kwa awamu ya pili hadi sasa umefika asilimia 54.
"Katika awamu hii ya pili, mradi umehusisha utoaji wa toleo kwenye bomba la inchi 16 linalopeleka maji katika mji wa Kisarawe na ulazaji wa bomba za inchi 8 kwa umbali wa kilomita 3.5 ambapo hadi sasa bomba zimelazwa umbali wa kilomita 2.1 na kazi bado inaendelea kwa kasi" amesema Mhandisi Richard.
Naye, Diwani wa Kata ya Kwembe Mhe. Nicholaus Batalingaya ameipongeza DAWASA kwa hatua ya mradi ilipofikia na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea na kusisitiza kulinda na kutunza miundombinu hii ili iendelee kuwanufaisha.
"Kwanza kabisa tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuweka huduma za jamii kipaumbele hasa huduma ya maji, pili niwapongeze DAWASA kwa kuendelea kutoa ushirikiano na viongozi katika kuhakikisha suluhu la maji katika kata yetu inapatikana. Tuwasihi Wananchi wa kata yangu na kata jirani tuendelee kuvumilia kwani changamoto ya maji inakwenda kuwa historia" amesema Mhe. Batalingaya.
Awamu ya kwanza ya maboresho ya mradi wa Maji Kwembe maduka tisa yalihusisha ulazaji wa bomba la inchi 12 kwa umbali wa mita 200 kutoka eneo la Kwembe maduka tisa hadi Shule ya sekondari Barbara Johanson na kukamilika kwa mradi wa huu kutanufaisha zaidi ya wateja 10,000 wa maeneo ya Malamba Mawili, King'azi A, King'azi B, Njeteni, Kwembe, Kwembe mpakani na Tawalani.