Na Elizabeth John _ NJOMBE.
WAFANYAKAZI wa sekta binafsi wakiwemo wa mashambani wamelalamika juu ya ujira duni na ucheleweshwaji wa mishahara kwa muda mrefu na sasa wamemuachia Rais Samia Suluhu Hassan awasaidie.
Pia changamoto ya kutopelekwa kwa michango ya kila mwezi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi hao imekuwa mwiba mkali unaowakatisha molari ya ufanyaji kazi.
Hayo yametajwa katika sherehe za mei mosi mkoani Njombe zilizofanyika katika viwanja vya sabasaba mjini hapa.
Aidha baadhi ya wafanyakazi wa mashambani akiwemo Jailan Abdalah mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa mashambani TPWU Sekta ya Kilimo na Frida Kidenya wamesema kilio kwa sekta binafsi kimekuwa kikubwa na kwa muda mrefu kwani ujira umekuwa kiduchu ukilinganisha na kazi wanazofanya.
Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omary amesema serikali ya mkoa imeendelea kuwapa stahiki zao wafanyakazi kwa wakati jambo lililosaidia kupunguza malalamiko.
Mkuu wa Mkoa was Njombe, Anthony Mtaka ametoa onyo kwa waajiri kuacha roho mbaya na hila dhidi ya watumishi wao badala yake wawe daraja .
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tucta Mkoa wa Njombe Mashaka Kisulila amesema siku ya wafanyakazi duniani ilianzishwa kutokana na manyanyaso ya wafanyazi na vibarua yaliyokuwa yakiwakumba wakiwa kazini.