Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema utekelezaji wa mipango na mikakati ya Serikali imekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji.
Ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 23.2 na kufikia Sh.trilioni 43.4 katika kipindi kilichoishia Aprili 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 35.2 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023.
Imesema jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 64.5 na kufikia Sh.trilioni 4.2 katika kipindi kilichoishia Aprili mwaka 2024, ikilinganishwa na Sh. trilioni 2.5 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023.
Hayo yamesemwa leo Mei 27,2024 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na na CPA Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Timiza(TIMIZA FUND) wa Kampuni ya Zan Securities Limited.
Akieleza zaidi CPA Mkama amesema thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja imeongezeka kwa asilimia 44.7 na kufikia Sh.trilioni 2.1 katika kipindi kilichoishia Aprili mwaka 2024, ikilinganishwa na Sh. trilioni 1.4 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023.
"Aprili 16, 2024, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) iliidhinisha Waraka wa Matarajio (Offer Document) na Mkataba wa Uendeshaji wa Mfuko wa Timiza. Idhini ilitolewa na CMSA baada ya Zan Securities Limited kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.
"Na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya uanzishaji na uendeshaji wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja. Napenda kutamka Timiza Fund ni mfuko ambao umekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Uwekezaji wa Pamoja.
"Timiza Fund ni mfuko unaoendeshwa na taasisi ya Zan Securities Limited ambaye ni Meneja wa Mfuko (Fund Manager) na Benki ya Mwanga Hakika ambaye ni Mtunza Dhamana wa Mfuko.
"Lengo kuu la Mfuko wa Timiza Fund ni kuhamasisha wawekezaji wadogo, wa kati, na wakubwa kuunganisha nguvu zao na kuwekeza kwa pamoja ili kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta ya fecha, hususan masoko ya mitaji,"amesema CPA Mkama.
Aidha, amesema malengo mahsusi ya Mfuko wa Timiza ni kuwawezesha watanzania wa kada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake, makundi maalum, taasisi na mifuko ya hifadhi ya jamii kunufaika na uwekezaji katika masoko ya fedha; kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza miongoni mwa watanzania; na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi.
Amefafanua kuanzishwa kwa Mfuko wa Timiza kunachangia utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kuwezesha wananchi kiuchumi.
Amesema katika hotuba yake kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 April 2021, Rais Samia alianisha kuwa mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ni kuendelea kuboresha Sera za Uchumi na Fedha.
Amesisitiza utekelezaji wa azma hiyo umeakisiwa katika miongozo ya Serikali inayolenga kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya umma na binafsi.
"Miongozo hiyo ni pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 2025/26 wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani kwa Maendeleo ya Watu; Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 2029/30; na Mpango wa Huduma Jumuishi za Fedha wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha ikiwa ni pamoja na masoko ya mitaji."
Aidha amesema katika juhudi za kuwezesha kufikia malengo ya kuanzishwa kwa mfuko huo CMSA imeidhinisha kushusha kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji kwenye Mfuko huu kutoka Shilingi milioni moja hadi Sh. 10,000.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwani itawezesha ushiriki wa wawekezaji wa kada mbalimbali katika Mfuko huu, ikiwa ni pamoja na wananchi wenye vipato vya chini, vya kati na vikubwa.
Pamoja na hayo amesema lengo la uwekezaji wa aina hiyo ni kuufanya mfuko kuwa na ukwasi unaotosha ili kukidhi mahitaji ya fedha za wawekezaji pindi mahitaji yanapotokea na kwamba
uwekezaji katika Mfuko wa Timiza una manufaa katika ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi hapa nchini.
Social Plugin