Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ELIMU INAYOTOLEWA NA TAWA YAMWOKOA MWANANCHI KUTOKA MDOMONI MWA MAMBA







Na Beatus Maganja, TAWA

Mkazi wa Kijiji cha Kasenyi kilichopo wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza Bw. Obeid Francis (44) amenusurika kuliwa na mnyamapori aina ya mamba baada ya kuikumbuka na kuitumia elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu inayoendelea kutolewa na Maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA maeneo mbalimbali nchini.

Akisimulia kisa hicho Obeid amesema tukio la kukamatwa na mamba huyo lilitokea oktoba 25, 2023 Kijiji cha Kasenyi majira ya jioni (saa 1 usiku) akiwa anaoga pembezoni mwa ziwa Victoria ambapo ghafla alishtukia amekamatwa mkono wa kushoto na mamba na kutupiwa ndani ya maji yenye kina kirefu na baadae kuibuliwa.

Kwa maelezo yake kitendo cha mnyama huyo kumuibua na kumrudisha majini kilirudiwa na mnyama huyo mara kadhaa na wakati anatafuta namna ya kujiokoa alikumbuka elimu iliyokuwa ikitolewa na Maofisa wa TAWA inayoelekeza kumchoma jichoni mnyama huyo kwa kutumia kidole pale ambapo mtu anapokuwa amekamatwa na mamba, na mara baada ya kufanya hivyo mamba huyo aliruka na kupotelea majini na yeye alijikokota kutoka majini akiwa amejaa majeraha.

"Nikiwa naoga majini, wakati ninageuka kwenda kuvaa nguo zangu ghafla nilishtukia upande wa mkono wa kushoto niliona kitu kikali kimenirukia, nilishtuka kikaanza kunizamisha ndani ya maji, kitu kizito na kinene, roho iliruka na kupata hofu kubwa, fikra zilinituma kwamba hapa tayari nimekamatwa na mamba" anaeleza Obeid Francis

"Liliponiibua likaanza kunipeleka kama umbali wa hatua tano kwenye maji marefu roho ikaniambia Sasa nimekufa, sasa nifanyeje? na usiku umeanza kuingia, lakini roho nyingine ikaniambia huwa wanasema mamba ukimkamata macho atakuachia, nilifanya hivyo na ndipo aliponiachia" ameongeza

Matukio ya wananchi kupata madhara yatokonayo na wanyamapori wakali na waharibifu hasa wale waishio pembezoni mwa maziwa na mito yamekuwa yakitokana na vitendo vya wananchi hao kufanya shughuli zao karibu na maji kama vile kuogelea/kuoga, kufua na kufanya uvuvi usio rafiki mambo ambayo yamekuwa yakihatarisha maisha yao.

TAWA imekuwa ikifanya jitahada endelevu za kutoa elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko maeneo mbalimbali nchini kwa wananchi ili kuwapatia mbinu za kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na wanyamapori hao na inasisitiza wananchi kuzingatia elimu hiyo ili waendelee kuwa salama.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com