Dar Es Salaam Tanzania, 14 Mei 2024
Foundation for Civil Society (FCS) na TradeMark Africa wamesaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha mazingira wezeshi na jumuishi ya kibiashara kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika uendeshaji wa biashara, kukabiliana na changamoto kubwa za kimfumo katika biashara na changamoto ya tabia nchi kama sehemu ya kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi Tanzania.
FCS imepokea ruzuku ya bilioni 2.3 kutoka Trademark Africa kutekeleza mradi huo ambao umefadhiliwa na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Ireland, na Norway, wenye thamani ya dola za kimarekani 900,000, unaolenga kuunganisha nguvu za Sekta Binafsi na Mashirika ya kiraia ili kukuza ukuaji wa uchumi wa kijani.
Makubaliano hayo yamefanyika leo Mei 14, 2024, katika Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Justice Rutenge amesema kuwa Ulinzi wa mlaji ni muhimu katika soko la biashara la kitaifa na kimataifa, na kwamba ushirikiano wao na Trademark Africa ni hatua kubwa ya kulinda haki za mlaji na kuhakikisha faida za Biashara ni shirikishi.
"FCS inajukumu la kipekee kama AZAKI na ina uwezo wa kutumia vema ubobezi wake kushirikiana na Sekta Binafsi kushughulikia masuala muhimu ya uharibifu wa mazingira na ukosefu wa usawa wa kijamii" amesema Rutenge.
Aidha, ameongeza kuwa mradi huo pia unalenga kuweka mazingira jumuishi na endelevu ya Biashara kwa kuongeza fursa za kibiashara kwa makundi ya pembezoni, kushirikiana na Asasi za kiraia katika kushughulikia mahitaji yao, kukuza mazingira ya biashara rafiki, na kuimarisha ulinzi wa walaji.
"Mradi huu unalenga kuboresha ustahimilivu wa Biashara dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na hivyo kuchangia katika uendelevu wa muda mrefu wa uchumi wa Tanzania na uendelevu wa mazingira.
"Ushirikiano huu unawakilisha kielelezo cha jinsi ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi unavyoweza kushughulikia kwa ufanisi changamoto za kimfumo katika masoko, na kuunda njia za mazoea ya biashara jumuishi na endelevu" ameongeza Rutenge.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi kumi na minane ijayo, FCS itatekeleza mkakati katika sekta nyingi za biashara, ikilenga kupunguza athari za matumizi ya mazingira na kukuza ushirikishwaji katika manufaa ya kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Trademark Africa Elibariki Shammy amesema, Mradi huo ni muhimu kwa malengo ya kimkakati ya kuchochea ukuaji wa biashara ambao ni endelevu na shirikishi.
"Tunaamini kwamba kupitia ushirikiano huu wa kimkakati baina yetu na FCS, tunaweza kuleta matokeo chanya na makubwa katika kuboresha mazingira ya biashara jumuisha nchini.
"kuwawezesha wanawake ni jambo la maendeleo na kuwajumuisha katika biashara kunakuza uchumi na kuinua jamii nzima" amesema Shammy.
Kupitia ushirikiano huo wa Trademark Africa na FCS kwenye mradi huo kunaendeleza mfumo bora jumuishi wa biashara utakaokabiliana na changamoto za biashara za kimataifa.
Social Plugin