Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

INEC YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA KWAHANI




Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar utafanyika tarehe 08 Juni, 2024.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Bw. Kailima, R. K jijini Dodoma leo tarehe 02 Mei, 2024 imesema kwamba fomu za uteuzi kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo zitatolewa kuanzia tarehe 17 hadi 23 Mei, 2024.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 23 Mei, 2024 na kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo zitafanyika kuanzia tarehe 24 Mei, 2024 hadi tarehe 07 Juni, 2024.

Tume imetangaza uchaguzi huo mdogo kufuatia taarifa ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyomtaarifu Mwenyekiti wa Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya ubunge katika Jimbo la Kwahani.

Spika ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 49(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka, 2024.

“Kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 49(1)(b) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Tume imevikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huo mdogo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com