Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KILI CHALLENGE 2024 YAZINDULIWA KUONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

 

Na Nadhifa Omar, Tacaids. 

Kampeni maarufu ya kuchangisha fedha za UKIMWI ya Kili Challenge imezinduliwa kwa mwaka 2024 ikitarajiwa kukusanya Shilingi Bilioni mbili.

Ikumbukwe kuwa Kampeni ya Kili Challenge huratibiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita Gold Mine Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ambapo hufanyika Julai ya kila mwaka.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika Ijumaa Mei 24, 2024 jijini Dar es Salaam, Kaimu Kurugenzi TACAIDS, Jumanne Isango, amesema TACAIDS  inaendelea kuheshimu mchango mkubwa unaopatikana kupitia Kili Challenge na kwamba wataendelea kudumisha kampeni hiyo.

“Kwa niaba ya wafanyakazi na uongozi wa TACAIDS, Mgodi wa Dhahabu wa Geita(GGML), Kamati ya Kili Challenge na Bodi ya Wadhamini ya Kili Challenge na Serikali ya Tanzania tunawashukuru kwa kuendelea kuunga mkono mpango wa kupanda mlima Kilimajaro.

 Madhumuni ya kili challenge imekuwa ni kuchangisha fedha na uhamasishaji kwa VVU na UKIMWI.

“Kwa pamoja, tufanye mpango huu uendelee kuwa shirika la hisani la sekta ya umma na binafsi dhidi ya VVU na UKIMWI katika Afrika Mashariki, kwa mwaka huu tunatarajia kuwa kampeni hii itakusanya Shilingi bilioni 2, hivyo, tuendelee kuunga mkono,” amesema Isango.

Akizungumzia mgawanyo wa fedha hizo, Isango amesema: "Kila siku na kila mwaka, fedha hizi zinazopatikana kupitia mpango huu zimekuwa zikiendelea kuleta athari chanya kwa jamii zinazozunguka. 

Hadi sasa kupitia Kili Challenge, tumefanikiwa kuchangia zaidi ya Asasi 22 za ndani na taasisi kadhaa za serikali na kuwanufaisha mamilioni ya Watanzania.

“Hili limewezekana kupitia michango ya hisani na msaada kutoka kwa wadau mbalimbali wanaofanya kampeni hii kuwa mfano ambao sote tunajivunia,” alisema Isango.

Aidha;  Isango ambaye alimwakilisha Kaimu Mkurugenzi wa TACAIDS, Dkt  Jerome Kamwela, amemshukuru Balozi wa Marekani nchini, Balozi Michael Battle, kutokana a mchango mkubwa ambao umekuwa ukitolewa na PEPFAR.

"Uwepo wako hapa leo, Mheshimiwa Balozi, kunaashiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini. 

“Tunashukuru kwa msaada mkubwa kutoka kwa PEPFAR na Mashirika mengine yote ya Serikali ya Marekani kwa miongo kadhaa sasa tangu janga la VVU kuibuka katika nchi yetu, tunapoadhimisha miaka ishirini na mbili tangu kuanza kwa Kili Challenge," alisema Isango.

Hali ya VVU na UKIMWI nchini
Kuhusu hali ya VVU na UKIMWI nchini Tanzania, Isango amesema kuwa fursa hii hutoa mambo muhimu kuhusu hali ya VVU na UKIMWI katika nchi yetu.
Amesema kwa mujibu wa THIS 2022/2023, Tanzania ina WAVIU 1,548,000. Miongoni mwa watu wazima wenye umri wa miaka 15+, maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka yamepungua kwa asilimia 16.7, kutoka watu 72,000 (THIS 2016/17) hadi 60,000 (THIS 2022/23).

Akizungumza kuhusu wapandaji mlima amesema: "Kwa wapandaji wetu wachangamfu kwa mwaka huu, ambao wataziacha familia zao nyuma na kukabiliana na changamoto ya kupanda milima na miteremko ya Kilimanjaro, tunasema, 'ninyi ndio mnaleta mabadiliko, hivyo tunajivunia uamuzi wenu ambao unaleta furaha kwa watanzania wengine .

“TACAIDS itaendelea kuimarisha dhamira yake ya kuifanya Kili Challenge kuwa kipengele cha kudumu katika shughuli zetu za Tanzania, tunafungua mikono yetu kwa ushirikiano zaidi na kampuni zote ambazo zinawajibika kwa matumaini na mustakabali mzuri wa taifa hili,” amesema na kuongeza kuwa “Kwa pamoja, kuelekea kukomesha VVU na UKIMWI ifikapo 2030,” amesema Isango.

Awali, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti wa Masuala ya Uendelevu na Mambo ya Ubia (Afrika), Simon Shayo, amesema vikundi mbalimbali vimefaidika na kampeni hiyo, ikiwa ni pamoja na watoto wa Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma, ambacho pia kinawatunza watoto wengine walio katika mazingira magumu.

 "Kundi la kwanza la watoto waliokulia katika kituo hicho sasa wanasoma vyuoni, wakiwemo wawili wanaosoma digrii za udaktari," alibainisha Shayo.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Michael Battle, amesema kwasasa wako katika hatua ambayo uendelevu ndio ufunguo wa mafanikio ya muda mrefu ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana chini ya PEPFAR huku akisisitiza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano ya UKIMWI.

“Uendelevu ni muhimu kwa sababu kadhaa muhimu. Kwanza, PEPFAR haikukusudiwa kuwa suluhisho la kudumu; ilikusudiwa kushughulikia hitaji la dharura. Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti janga la UKIMWI. 
Viwango vya maambukizi mapya vimepungua kwa kiasi kikubwa, kama vile vifo vinavyohusiana na UKIMWI. 

“Pili, Tanzania iko kwenye njia nzuri kuelekea kuwa nchi ya kipato cha kati. Kwa maendeleo haya Tanzania itazidi kuwa na uwezo wa kushughulikia mahitaji yake ya afya.

 Moja ya vipaumbele vyangu kama Balozi wa Marekani nchini Tanzania imekuwa ikiimarisha uhusiano mkubwa wa kibiashara ili kufikia malengo yetu ya pamoja. Nina furaha kuona ushirikiano uliopanuliwa kati ya sekta ya afya ya Marekani na Tanzania. 

Sekta ya binafsi itakuwa muhimu katika awamu inayofuata ya juhudi zetu za kuzuia na matibabu ya VVU/UKIMWI,” amesema Balozi Battle.

Ameongeza kuwa, uendelevu ni kuhusu Tanzania kuongoza katika mipango yake ya afya. Kwa kudumisha mafanikio yaliyopatikana kupitia PEPFAR, itazuia kuibuka tena kwa VVU/UKIMWI kama tishio kubwa kwa afya ya umma. 

“Ni muhimu kwamba Tanzania iendelee kuendeleza programu muhimu ambazo PEPFAR imefadhili kwa miaka 21 iliyopita. Mpito huu sio tu juu ya ufadhili lakini juu ya kukuza hisia ya uhuru na uwajibikaji wa kifedha,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Geita Gold Mining Limited (GGML),  Duan Archery, alieleza furaha yake kwamba makampuni mengi yamehudhuria hafla ya kuchangisha fedha hapa Dar es Salaam.
"Michango yenu ni ya thamani kubwa na itatusaidia kufikia lengo letu la 'kufikia sifuri'," amebainisha.

Malengo matatu ya sifuri ni kutokuwepo kwa maambukizi mapya, kutokuwepo kwa ubaguzi, na kutokuwepo kwa vifo vinavyohusiana na UKIMWI. 


Kwa mujibu wa Archery, mwaka huu wanatarajia kuwa na washiriki 60: wapandaji mlima 42 na waendesha baiskeli 18. Wawili kati ya washiriki hawa ni watoto wadogo, mvulana na msichana kutoka Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma cha Geita, ambacho kilianzishwa mwaka 2006 kwa ufadhili kutoka Kilimanjaro Challenge. 

Kili Challenge inavyofanyika
Kilimanjaro Challenge ilianzishwa mwaka 2022 chini ya uratibu wa  Geita Gold Mining Limited (GGML) na Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania _TACAIDS kwa lengo la kuchangisha fedha za Mwitikio wa UKIMWI. 

Fedha hupatikana kutokana na  kupanda na kuzunguka Mlima Kilimanjaro kila mwaka. Washiriki hununua tiketi za Challenge kama sehemu ya kampeni yao ya kuchangia fedha.

Wakati baadhi ya ada inagharamia kupanda mlima na kuendesha baiskeli, sehemu kubwa ya fedha inaingia kwenye Kili Trust Fund, na hutumika kusaidia mapambano ya kitaifa dhidi ya UKIMWI. Mfuko wa Kili ni mchangiaji mkuu wa Mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com