Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza kuwa timu ya watalaamu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) na Makandarasi itatumia saa 72 (siku 3) kukamilisha zoezi la kurejesha miundombinu ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam, ambayo imeharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zilizombatana na kimbunga Hidaya.
Amesema hayo Mkoani Lindi Mei 05, 2024, mara baada ya kuwasili na kukagua uharibifu wa miundombinu ya barabara ya Lindi - Dar es Salaam na kuzungumza na wananchi na wasafiri wa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na Dar es Salaam wanaotumia barabara hiyo na kutoa pole na kuwataka kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kujereshwa miundombinu.
“Mitambo ipo inaletwa hapa, kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii itaanza wakati wowote kuanzia sasa, ni lazima tuanze na kipande kimoja ili tuweze kufika katika maeneo mengine yaliyoathiriwa. Namna miundombinu imeharibika na tathmini iliyofanyika tunahitaji masaa yasiyopungua 72 ili kuweza kurudisha mawasiliano,” amefafanua Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa mawasiliano ya barabara hiyo yamekatika katika maeneo matano ambayo ni pamoja na eneo la barabara ya Somanga – Mtama, eneo la Mikereng’ende kutokea Somanga na eneo la Lingaula kutokea Lindi.
Aidha, Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itafanya kila jitihada ili ifikapo Jumatano jioni mawasiliano ya barabara hiyo yarejee katika hali yake.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo ameeleza kuwa maji yaliyokuwa yakipita juu ya barabara yalizidi kiwango na kusababisha madaraja kushindwa kuhimili wingi na kasi ya maji na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo matano ikiwemo Somanga, Mikereng’ende, na Lingaula.
Nyundo amemueleza Waziri Bashungwa kuwa kazi ya awali iliyofanyika ni kuwasiliana na taasisi zinazohusika kwa Mkoa wa Ruvuma, Mtwara na Lindi ili kutoa taarifa kwa wasafirishaji na watumiaji wa barabara hiyo kusimamia safari zao mpaka pale miundombinu itakaporejeshwa katika hali yake.