Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MNADA WA MHUNZE KUFANYIWA UTAFITI WA KINA UWEPO WA TOPE MAJI - PROF. MUSHI


Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mchakato wa kufanya Utafiti wa kina juu ya chanzo cha tope maji yatokayo katika ardhi ndani ya mnada wa Mhunze Wilayani Kishapu ikiwa ni njia mojawapo ya kujua athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa hali hiyo katika eneo la ujenzi ambao unaendelea katika Mnada huo ili kuweza kutafuta suluhisho. Hii ni kufuatia hali hii kuleta taharuki kwa wafugaji na wauzaji wa mifugo kwenye mnada huo.

Akizungumza, leo Mei 29, 2024 Wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga wakati akienda kukagua hali ya eneo la mnada wa Mhunze, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Daniel Mushi amesema Wizara imeamua kufanya Utafiti wa kina ili kujiridhisha kama hali ya mnada wa Mhunze ni salama na kukabiliana na uwepo wa tope kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa watu na mifugo kwenye mnada huo.

"Leo tumekuja na wataalam kutoka Taasisi ya madini Tanzania kwa ajili ya kupima kilichotokea na kutupa taarifa, ambapo mpaka sasa wameshafanya uchunguzi wa awali na wametueleza kisayansi ni kitu gani kina sababisha matope haya na kutuhakikishia kwamba mradi wa ujenzi wa ukuta unaozunguka eneo hili na maboresho mengine yanaweza kuendelea", amesema Prof. Mushi.

Aidha, Prof. Mushi alisema Wataalamu watakapofanya uchunguzi wa kina wataeleza namna ya kukabiliana na suala hili ili yasijitokeze madhara na wataalamu wameihakikishia Wizara kuwa hakuna madhara yanayoweza kusababisha maafa katika mnada huo wa Mhunze.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude amesema mbali na utafiti huo lakini pia yapo marekebisho na maboresho yanayotarajiwa kufanywa kwenye eneo hilo la mnada na maeneo ya pembezoni ili kujihakikishia usalama wa wananchi na mifugo.

Vilevile Mhe. Mkude ameishukuru sana Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuja kwa wakati na watafiti ili kufanya utafiti baada ya kusikia jambo hili la kufurika kwa tope katika mnada wa Mhunze.

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo la kufurika kwa tope katika mnada wa Mhunze, Mjiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini Tanzania, Bw. Sudian Chilagwile amesema, sababu iliyofanya waitwe na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuja kufanya uchunguzi kwenye eneo la mnada wa Mhunze ni uwepo wa chemchem ya maji tope na udongo uliojaa matope ukitoka chini ya ardhi.

Bw. Chilagwile, ameweka bayana kuwa wao kama watafiti watafanya kazi ya Utafiti katika eneo hilo la mnada ili kubaini chanzo, japo utafiti wa awali wa kisayansi unaonyesha sababu ya yote ni uwepo wa mvua nyingi ambazo zimeleta athari katika miamba iliyopo aridhini ambayo imesababisha uwepo wa tope hilo, na kubainisha kuwa jambo hili haliwezi kuathiri shughuli za mnada huo kuendelea, ila watatoa ushauri kwa Wizara na wakandarasi juu ya ukarabati wa eneo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com