NBS YATAJA SABABU ZA VIASHIRIA VYA KIUCHUMI KUIMARIKA, YAELEZA MWENENDO WA UZALISHAJI NISHATI, WATALII

 


Na Dotto Kwilasa,Malunde Blog 1,Dodoma

KUFUATIA mwenendo wa viashiria vya kiuchumi vya muda mfupi kuanzia January hadi Machi 2024 ambao unatajwa kuimarika,mwenendo wa uzalishaji wa Nishati ya umeme umeendelea kuimarika hadi saa za kilowatt bilioni 2.7 kutoka saa za kilowatt bilioni 2.5 kwa kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la saa za kilowatt milioni 236.8 sawa na asilimia 9.5.

Hayo yalielezwa na Daniel Masolwa Mkurugenzi wa takwimu za uchumi kutoka ofisi ya taifa ya Takwimu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa viashiria vya kiuchumi vya muda mfupi kwa kipindi cha mwezi januari hadi machi 2024.

Masolwa ameeleza kuwa kiasi kikubwa cha umeme uliozalishwa katika kipindi hicho mwaka 2024 kimetokana na gesi  asilia kwa asilimia 65.0 , chanzo cha maji asilimia 33.6 na mafuta kwa asilimia 1.4 . 

"Uzalishaji wa umeme kwa aina ya chanzo katika kipindi cha January hadi Machi 2023 ulikuwa chanzo cha gesi asilia asilimia 73.5,chanzo cha cha maji asilimia 25.7 na chanzo cha mafuta asilimia 0.8," ameeleza

Katika hatua nyingine Masolwa ameeleza idadi ya watalii walioingia nchini kuwa iliongezeka hadi 520,324 katika kipindi cha januari hadi machi 2024,ikilinganishwa na watalii 409,082 walioingia nchini katika kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la watalii 111,242 sawa na asilimia 27.2

Amesema kuwa idadi ya watalii walioingia nchini mwezi machi 2024 iliongezeka hadi 155,810 ikilinganishwa na watalii 118,186 walioingia nchini  mwezi machi 2023 ikiwa ni ongezeko la watalii 37,624 sawa na asilimia 31.8

Aidha idadi kubwa ya watalii walioingia nchini kutoka nje ya bara la afrika walitoka Italia,ufaransa na marekani,wakati idadi kubwa ya watalii kutoka katika Bara la afrika walitoka Burundi,Kenya na Zambia.

Kwa upande wa huduma ya mawasiliano ameeleza kuwa imekuwa ni kichocheo kikubwa cha shughuli mbalimbali za kiuchumi Tanzania na dunia kwa ujumla, ambapo katika kipindi cha januari hadi machi 2024 huduma ya mawasiliano iliendelea kuongezeka hadi dakika za kuongea bilioni 34.96 kutoka dakika bilioni 32.04 kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la dakika bilioni 2.93 sawa na asilimia 9.1


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post