Wananchi mbalimbali wakipata maelezo kutoka kwa Wataalamu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal Tanga.
........
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imeudhihirishia umma kuwa, taaluma kwa jamii na viwanda ni nguzo muhimu katika kutatua changamoto na kukuza uchumi wa viwanda kupitia ubunifu.
Maoni hayo yametolewa na Msanii wa Muziki wa dansi Mrisho Mpoto alipotembelea Banda la Taasisi hiyo Mei 30, 2024 katika maonesho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal, Bombo Jijini Tanga .
"Naipongeza taasisi ya Nelson Mandela kwa kutoa taaluma inayotatua changamoto za jamii kupitia bunifu na tafiti mbalimbali zinazozalishwa na wanataaluma wake" amesema Mrisho Mpoto
Anaongeza kwa kueleza kuwa amejifunza mengi ikiwemo ubunifu wa funza lishe , Uji Tayari wenye virutubisho na madini muhimu, Dawa ya Asili ya Kuchakata Ngozi , Mtambo wa kutengeneza gesi asilia na kuchuja majitaka na Chujio la Maji safi la NanoFilter.
Kwa upande wa wananchi wengine waliopata fursa ya kutembelea banda hilo , wameeleza kuwa, taasisi hiyo inatekeleza kwa vitendo sera mpya ya elimu kwa kuonesha kuwa, mbali na taaluma , ujuzi na ubunifu ni vitu muhimu katika mchango wa maendeleo ya nchi.
Mbali na bunifu hizo , Taasisi inatoa huduma zingine ikiwemo ushauri wa bure kwa wananchi kuhusu namna bora ya kufanya utafiti utakaoibua bidhaa za ubunifu kupitia Kituo Atamizi (Incubation Centre) ambacho huatamia wabunifu wa ndani na nje ya taasisi kwa lengo la kuibuka na bunifu zitakazotatua changamoto za jamii.
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ni taasisi iliyojikita katika kufanya tafiti na kutoa Taaluma katika ngazi ya Umahiri na Uzamivu iliyopo Tengeru jijini Arusha
Msanii wa Muziki wa Dansi Mrisho Mpoto akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela katika maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal Tanga.
Mbunifu kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Aziza Konyo ( kulia) akifafanua jambo kwa Wananchi waliotembelea banda hilo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal Tanga.
Wananchi mbalimbali wakipata maelezo kutoka kwa Wataalamu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal Tanga.
Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ubunifu Prof Anthony Mshandete akiwa katika picha ya pamoja na wabunifu na watafiti kwenye maadhimisho ya wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal Tanga.