Na. Mwandishi Wetu – Geita
SERIKALI imesema itaendelea kuchukua hatua za dhati kuwalinda watu Wenye Ualbino ikiwemo kuwafikisha katika vyombo vya dola watakaobainika kuwafanyia ukatili.
Hayo yamesemwa Mei 12, 2024 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi kufuatia tukio la shambulio la mtoto mwenye Ualbino lililotokea tarehe 4 Mei, 2024 katika kijiji cha Mtakuja, Katoro Mkoani Geita.
Aidha, Mhe. Ummy amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inakemea kitendo hicho kisichokua na utu na inawaasa wananchi kusaidia kudhibiti vitendo hivyo kwa kuimarisha ulinzi ndani ya familia na jamii inayowazunguka.
Vile vile, Mhe. Ummy amezitaka Kamati za Ulinzi na Usalama nchini kuhakikisha vitendo vya aina hiyo vinadhibitiwa, na Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) kuelimisha jamii kuhusu haki za Watu wenye Ualbino.
Kwa upande mwingine, Mhe, Ummy ametoa pole kwa familia ya mtoto Kazungu Malecha (Mwenye Ualbino) kwa shambulio hilo lililotokea na tayari Ofiisi hiyo imefanya mawasiliano na Wizara ya elimu kwa ajili ya mtoto huyo kusomea shule ya bweni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Godson Mollel amesema anaungana na wadau wengine wa haki za binadamu kupinga kitendo cha kikatili alicho fanyiwa mtoto huyo.
Naye, Kaimu Mganga Mkuu Geita Dkt. Stephen Mwaisombwa amesema hali ya mtoto huyo kwa sasa ni nzuri kutokana na matibabu aliyo patiwa na anatarajiwa kuruhusiwa muda wowote.