SERIKALI KUJA NA MIKAKATI YA KUPIMA UBORA WA ELIMU NCHINI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ,akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya Tathimini ya ujifunzaji na ufaulu wa Wanafunzi .

................

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali inaweka mikakati ya kuendelea kupima ubora wa elimu kwa kuzingatia vigezo Kitaifa na Kimataifa.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Mei 30, 2024 jijini Tanga wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya Tathimini ya ujifunzaji na ufaulu wa Wanafunzi ambapo amesema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuongeza ubora wa elimu na kwamba suala muhimu ni kujipima Kitaifa na Kimataifa.

Ameongeza kuwa mageuzi ya elimu yaliyofanyika yana maana pana na yameleta mfumo tofauti wa elimu nchini na kwamba ni muhimu kuwa na tathimini ili kuhakikisha elimu inayotolewa ina kuwa bora .

"Suala la kuwa na tathimini ya kweli ni muhimu, tunahitaji mfumo wa mtihani wenye weledi na uadilifu ili tuwe na uhakika wa tunachopata katika matokeo yake" amesema Waziri huyo.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa taarifa hiyo inatoa picha halisi kuhusu ufundishaji na ujifunzaji katika Shule za Msingi na Sekondari ambapo mapendekezo yaliyotolewa yanaonesha dira ya nini cha kufanya katika kuimarisha ufundishaji na tathimini katika ngazi ya Shule za Msingi na Sekondari.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kushirikiana na wadau wa elimu katika kuhakikisha masuala ya ufundishaji, ujifunzaji na tathmini katika shule yanaimarishwa kwa lengo la kukuza umahiri wa wanafunzi katika masomo.

Awali akiwasilisha Taarifa ya Tathimini ya Ujifunzaji na Ufaulu wa Wanafunzi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Said Mohamed amesema kuwa kuanzia Mwaka huu hakutakuwa na maswali ya kuchagua katika mitihani ya Hisabati.

Dkt. Mohamed amesema kuwa tayari mafunzo yameshatolewa kwa ajili ya kutekeleza hilo.

Amebainisha kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ililiagiza Baraza kufanya tathimini ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa Wanafunzi katika masomo ya Hisabati, Bailojia, Fizikia na Lugha ya Kingereza ili kuja na mapendekezo ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post