Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIPA TANROADS BIL 6.5 KUKABILIANA NA ATHARI ZA MVUA ZA EL-NINO MKOANI RUKWA


Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya matengenezo ya dharura ya kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja ambayo yameharika kutokana na mvua kubwa za El-nino zilizonyesha kwa wingi Mkoani Rukwa.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kukubali kutoa kiasi hicho cha fedha ambacho kimewezesha kurejesha miundombinu iliyoharibiwa.

Mhandisi Mwanga amesema hayo tarehe 6 Mei 2024 baada ya kutembelea na kukagua miundombinu iliyoharibika ikiwa ni pamoja na Daraja la Solola lililopo barabara ya Ilemba – Kaoze ambapo barabara unganishi ilisombwa na maji na hivyo kufanya upana na kina cha mto kuongezeka.

Pia amempongeza Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta na Viongozi wengine wa Wizara, TANROADS na Serikali kwa maelekezo, usimamizi wa karibu na msukumo wa pamoja kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa haraka.

Amesema kwa ujumla maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hizo zilizonyesha Mkoani humo kuanzia mwezi Disemba 2023 hadi Aprili 2024 ni Barabara ya kutoka Kasansa – Muze hadi Kiliamatundu ambako jumla ya madaraja takribani 18 yalipata athari kati ya hayo madaraja 6 ndio yaliyoharibika zaidi.

“Tangu tumepata athari ya mvua hizi tumekuwa tukifanya matengenezo endelevu ya kuhakikisha kwamba kila kunapotokea athari barabara inafunguka na magari yanapita, tumeendelea kufanya hivyo na mpaka sasa Serikali imeshatuletea shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya kufanya marekebisho na kufungua njia pale ambapo inapojifunga’’ amekaririwa Mhandisi Mgeni na kuongeza kuwa

“Kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Aprili - 2024, Mvua imepungua kwa hiyo tumeanza kufanya maboresho ya muda wa kati, tunarudishia madaraja ambayo yamebomoka na mpaka sasa hivi zile barabara unganishi ambazo madaraja hayakusombwa na maji tumeshazirudishia na barabara zinapitika vizuri’’

Mhandisi Mgeni ametoa wito kwa watumiaji wa barabara hasa wakati huu wa mvua kuwa na subra na kuongeza umakini pale ambapo wanaona maji yamepita juu ya barabara au daraja ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Naye Msimamizi wa Kitendo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Rukwa Mhandisi Galasiano Tovagonze amesema kutokana na athari hizo wamefanikiwa kufanya manunuzi ya Wakandarasi 7 ambao wanafanya kazi ya matengenezo ya muda wa kati.

Ameongeza kuwa Wakandarasi wawili wapo katika barabara ya kutoka Kasansa – Muze, Mkandarasi mmoja yupo kipande cha Muze – Mtowisa na Wakandarasi wanne wapo kipande cha Mtowisa -Ilemba, wote wanafanya kazi ya kurejesha miundombinu iliyoharibika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com