Wakala ya barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Lindi umefanikiwa kurejesha mawasiliano yaliyokuwa yamekatika kati ya Kilwa Masoko-Nangurukulu wilaya ya Kilwa na wilaya ya Liwale mkoani Lindi.
Mawasiliano hayo yamereshwa ndani ya saa 24 kupitia kazi iliyofanyika usiku na mchana hadi kuhakikisha daraja la muda katika mto Zinga ambao unatenganisha kijiji cha Zinga na Miguruwe linatengamaa ili shughuli za usafirishaji wa abiria na mazao ya chakula na biashara ziweze kuendelea.
Daraja hilo lilisombwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo uliosababishwa na kimbunga Hidaya kilichotokea Mei 3 na 4, 2024 katika mkoa wa Lindi na Mtwara.
Kurejea kwa mawasiliano hayo ni kama kurudisha matumaini ambayo watu walikuwa wameyapoteza kwani hiyo ndiyo njia pekee waliyokuwa wakiitegemea kufikisha mazao yao sokoni na hata bidhaa za kutumia majumbani.
Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi Mhandisi Emil Zengo amesema kimbunga hidaya kilipopita maji yaliongezeka wingi na kasi kiasi cha kupita juu ya daraja hilo.
“Daraja hili liliweza kusukumwa kabisa, kusogea pembeni na kuta zake kubomolewa, kimbunga hiki ndiyo pia kilisababisha athari katika maeneo mengine pia ya barabara zetu ambayo ni barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kuja Lindi hadi Mtwara,” amekaririwa Mhandisi Zengo
Kwa sasa eneo hilo limekamilika na barabara ya kutoka Liwale hadi Nangurukulu inapitika huku matengenezo madogo madogo katika baadhi ya maeneo yakiendelea kufanyika ili wananchi waweze kupita na kufurahia uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita.
Mbali na daraja hilo, kimbunga Hidaya kilipopita nchini, pia kilisababisha zaidi ya madaraja manne kukatika yakiwamo ya Somanga, Songas, Mikereng'ende, na la Mto Matandu, huku baadhi ya vijiji vikizingirwa na maji.
Baadhi ya wananchi wameeleza furaha yao juu ya kurejea kwa mawasiliano huku wakielezea adha waliyokuwa wakiipata awali ikiwemo kukosa mahitaji muhimu.
Kwa nyakati tofauti walipotoa maoni yao waliishurukuru Serikali kwa kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida.
Mary Mwela mkazi wa Miguruwe, Mwajuma Kassim Kibweku mkazi wa Miguruwe na Mjumbe wa Serikali ya kijiji, Fadhil Hemed Ngulile mkazi wa Miguruwe, Nurdin Maiki diwani wa kata ya Njinjo, Abdul Sadick dereva wa basi, Hemed Kingwande mwenyekiti kijiji cha Miguruwe wametoa shukrani zao kwa Rais wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za dharula kwa ajili ya kurejesha mawasiliano ya barabara.
Kwa upande wake Msimamizi wa barabara ya Kilwa Masoko-Nangurukuru-Liwale Mhandisi Anna Nnko amesema Mbali na daraja hilo pia ipo sehemu ya barabara hiyo ilimegwa na maji yaliyosababishwa na mvua kubwa za El-Nino zilizokuwa zikinyesha jambo ambalo lilifanya TANROADS kulazimika kuihamishia upande mwingine ili shughuli za kiuchumi ziweze kuendelea.