TBS KANDA YA ZIWA YATEKETEZA TANI SABA YA BIDHAA ZISIZOKIDHI MATAKWA YA VIWANGO


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa limeteketeza tani saba ya bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango ikiwemo vipodozi vyenye viambata sumu, maziwa ya watoto na vyakula mara baada ya kufanya ukaguzi kwenye masoko katika kanda hiyo.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Afisa udhibiti ubora Mwandamizi TBS, Nuru Mwasulama amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu na huwa yanafanyika kwa kushitukiza nchi nzima.

Amesema lengo la TBS ni kukuza biashara nchini lakini wanataka watu wafanye biashara ambazo ni za halali na haki bila kuleta athari ya afya kwa mtumiaji wa bidhaa.

"Kazi ya TBS sio kukamata na kuteketeza bali wanajenga uelewa kwa wadau mbalimbali na kutoa elimu, na moja ya vipodozi tulivyoteketeza ni matokeo ya wateja kutoa taarifa". Amesema

Kwa upande wake Afisa udhibiti ubora TBS, Deus Mlenga ametoa wito kwa wananchi wanapoona bidhaa zozote zile ambazo zimeisha muda wa matumizi na bidhaa ambazo zina viambata vya sumu waweze kutoa taarifa kwa wakati .

Aidha amewaasa wananchi kuwa makini na ununuaji wa bidhaa sokoni ikiwemo chakula kuangalia tarehe ya za kutengenezwa na tarehe za kuisha muda wake lakini vilevile na kuangalia kwenye mitandao ya kijamii bidhaa ambazo zimepigwa marufuku kwamba si salama kwa matumizi ya binadamu.

Madhara ya kutumia bidhaa za vipodozi vilivyopigwa marufuku ni pamoja na kuongezeka kwa saratani, matatizo mengine ya kiafya pamoja na kuathirika kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post