|
Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo Mobhare Matinyi. |
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo Mobhare Matinyi ameongoza jopo la wadau wa Habari kufanya utalii wa majengo ya kimkakati yanayojenga katika Jiji la Dodoma ikiwemo jengo la Stesheni ya reli ya kisasa – SGR Mkonze.
Miradi mingine ni pamoja na Mji wa Kiserikali uliopo Mtumba Dodoma pamoja na Ujenzi wa uwanja wa Ndege wa kisasa wa Msalato ambao sehemu ya kwanza ya mradi huo unaojengwa na Mkandarasi M/s Sinohydro Corporation Ltd ambao unahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya magari, uzio na mfumo wa maji unaendelea vizuri.
Ziara hiyo imekuja mara baada ya kukamilika kwa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo May 3 ikiwa ni maadhimisho ya miaka 31 huku vikiangaziwa kuzingatia maadili katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Matinyi ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kukamilisha ujenzi wa majengo ya mji wa serikali mtumba,uwanja wa ndege wa Kimataifa wa msalato pamoja na Mradi wa Treni ya umeme.
Aidha Msemaji mkuu huyo wa serikali ameweka wazi kuwa utekelezaji wa Miradi hiyo ni kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweka mkazo katika maendeleo.
Kwa upande wake Mratibu wa kuhamishia shughuli za serikali Dodoma chini ya uratibu wa ofisi ya waziri Mkuu Meshack Bandawe amesema mradi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa msalato utaongeza idadi ya ndege ikiwemo ndege zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 kwa wakati mmoja.
“Kwenye mradi huu sehemu hii tumeona unaenda vizuri, japo tupo nyuma kidogo lakini tumeona juhudi za Mkandarasi kwa hiyo hilo halitakuwa tatizo katika kuweza kufidia huo muda ambao umepotea,”amesema
Nao baadhi ya wandishi wa Habari waliotembelea Miradi hiyo akiwemo mjumbe wa Bodi yaTaasisi ya vyombo vya Habari kusini mwa Africa tawi la Tanzania (MISA) Ida Mushi pamoja na Mwenyekiti wa chama Cha waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha Cloud Gwand wameiomba serikali kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa muda uliopangwa.
Waandishi wa Habari kutoka Mikoa Mbalimbali nchini wametembelea miradi hiyo kwa lengo la kuona namna serikali inavyotekeleza miradi hiyo ambapo wameahidi kuyasema mazuri hayo yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin