Wananchi na wakazi wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wamejitokeza kwa wingi katika hospitali ya wilaya ya Kasulu kupata huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kigoma Maweni, ambao wamepiga kambi ya siku nne mfululizo.
Wakizungumza wananchi hao wameiomba serikali na Taasisi binafsi kuwa na utaratibu kwa kuwawekea kambi ya madaktari bingwa kama hao angalau mara moja kwa mwezi ili waweze kupata huduma za kitatibu na kupunguza gharama za kusafiri kufuata huduma hizo.
Hatua hiyo imekujamara baada ya Majey Foundation wakishirikiana na Taasisi ya LALJI Foundation, Game Frontiers na Hiltop kufadhili ujio wa madaktari hao na kwamba kuwepo kwa huduma hiyo katika maeneo yao kunapunguza muda wa kufuata huduma na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali.
Mkazi wa Kasulu mji, Juma Bujuibili amesema wananchi wengi wanaishi maeneo ya vijijini na vipato vyao vya chini kuweza kumudu gharama za kufuata huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa hivyo wengi kujikuta wakiathirika na kupoteza maisha kwa kukosa matibabu ya kibingwa.
“Wananchi wengi vipato vyetu ni vya chini na tunategemea kilimo kuendesha maisha yetu hivyo hatuwezi kumudu gharama za kusafiri kwenda nje ya wilaya au mkoa kwaajili ya kupata huduma za kibingwa na tunaopata shida zaidi ni sisi ambao tumeshakuwa watu wazima, hivyo niombe serikali iweze kutufikiria katika hili,”amesema Bujuibili.
Naye Yona Kazamaso amesema wananchi wengi wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali lakini wanashindwa kusafiri na kufata huduma za kibingwa kwa kuhofia gharama kuwa kubwa lakini uwepo wa kambi hiyo ya siku tano ya madaktari bingwa wengi watanufaika kwa kupata vipimo na matibabu bure.
“Nimefika kupata matibabu baada ya kupata taarifa za uwepo wa kambi hii nimefurahi kwani awali ilitulazimu kusafiri hadi Bugando au Kigoma mjini kupata huduma za kibingwa, amesema Mkazi wa Kilimani, Grace Benedict
Mwenyekiti wa LALJI Foundation, Imtiaz Lalji amesema wameamua kufadhili kambi hiyo ya madaktari kusaidia kuboresha afya za wana Kigoma kwa kuhakikisha wanapata vipimo na matibabu bure na kwamba wanamefanya hivyo kwasababu familia yao wote ni wazaliwa wa mkoa wa Kigoma.
“Tumekuwa tukizunguka mikoa mbalimbali nchini kutoa huduma hizi lakini tumeona mkoa wa Kigoma una uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa tunaenda kujipanga ili kuweza kurudi kwa mara ya pili,”amesema Mkurugenzi wa Game Frontiers, Mohammed Taki
Daktari bingwa wa Upasuaji, Frank Sudai amesema wagonjwa wengi aliowapokea wamebainika na tatizo la shinikizo la juu la damu ambalo linatokana na mfumo wa maisha na ulaji usiozingatia lishe bora.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Semistatus Mashimba amesema wananchi zaidi ya 1800 kwa siku nne kati ya tano wamejitokeza kupata huduma hizo za kibingwa na wameweza kubaini wananchi wengi wanauhitaji huduma hiyo ya kibingwa mara kwa mara.
“Sisi kama serikali tutaenda kuliangalia jambo hilo kwa kushirikiana na wadau ili kuwe na utaratibu wa uwepo wa kambi kama hii ili kuwapunguzia mzigo wa gharama kwa wananchi ambao wengi wao ni wakipato cha chini ambao hawaweze kumudu kufata hudama za kibingwa katika hospitali za rufaa,”amesema Mashimba
Social Plugin