Siku chache baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/25, na kuahidi kuongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi kutoka 223,201 hadi 252,245 baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu wameonekana kuguswa na jambo hilo.
Akitoa maoni yake juu ya suala hilo, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Samwel Alfred amesema kuongezeka kwa kwa kiasi hicho cha fedha kutasaidia kuinua vijana wengi wenye nia njema ya kujiendeleza kimasomo lakini wana uwezo duni wa kifedha lakini pia itasaidia Tanzania kuimarika kwa kuwa na vijana wengi walioelimika.
Serikali imeahidi kutoa mikopo kwa wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ambapo shahada ya kwanza 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na SAMIA Skolashipu 2,000.
Aidha itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 40 wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi hususan wanafunzi wa kike waliohitimu mtihani wa taifa wa kidato cha Sita na shahada ya awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.