NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo wameipongeza Serikali kuongeza fedha katika bajeti ya Elimu kwa mwaka wa fedha 2024-2025 ambapo itawapatia fursa wanafunzi waliokosa fedha kwa ajili ya kujiendeleza kwenye masomo ya elimu ya juu kwa kuwapatia mikopo ambayo itawasaidia kufikia ndoto zao.
Kwenye Bajeti hiyo serikali imetenga fedha za kitanzania Trilioni 1.97 ambazo ni ongezeko la asilimia 17.
Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 22, 2024 na wadau hao katika semina za Jinsia na Maendeleo zinazofanyika kila Jumatano katika ofisi za TGNP -Mtandao Jijini Dar es Salaam, ambapo wamechambua bajeti ya Wizara ya Elimu na kugundua kuwa ungizwaji wa masuala ya kijinsia umewekwa kwa uchache.
Akizungumza katika semina hiyo, Mchambuzi na Mtafiti wa masuala ya Jinsia Jofrey Chambua amesema Wizara ya Elimu imejitahidi kwa kiasi fulani kufanya ukondoishaji wa masuala ya kijinsia ingawa kama nchi safari bado ni ndefu kwani haijaangalia kwa undani kutizama suala la jinsia,wanawake na wanaume pekee yao.
"Tunatoa wito kwamba tafiti zinazofanyika serikali iiangalie mnyambuliko wa kijinsia katika maeneo ya vijijini na mijini,lakini kuangalia kundi lengwa katika tafiti husika ziwezekufanya masuala ya ukondoishaji" amesema Chambua
Aidha wadau hao wameiomba serikali kuhuisha sera na miongozo ya Elimu na mafunzo nchini kwa kushirikisha jamii pamoja na kujumuisha masuala ya ukondoishaji wa kijinsia.
Pamoja na hayo, Chambua amebainisha kuwa makundi maalumu wakiwemo viziwi na walemavu wanahitaji miundombinu rafiki na nyenzo za kuwasaidia hasa katika kipindi hiki cha mageuzi ya sayansi na Teknolojia.
Chambua ametoa wito kwa wanafunzi wanaopata fursa ya kusoma kupambana kupata elimu ambayo itawasaidia kujitambua na kujikomboa katika masuala ya kiuchumi na kusaidia jamii inayowazunguka.
Social Plugin