Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUPAMBANA NA CHANGAMOTO YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU


-Waipongeza TAWA kwa ushirikishaji

Na. Beatus Maganja

Kufuatia changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini, wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa hususani Shinyanga na Mwanza wamekubali na kuahidi kushirikiana na Serikali kukabiliana changamoto hiyo ili kupunguza adha kwa wananchi hasa wale wanaoishi pembezoni mwa hifadhi.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ziara iliyofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania -TAWA katika Mikoa ya Kanda ya ziwa, wananchi hao wameelezea adha kubwa wanayoipata kutokana na changamoto itokanayo na wanyamapori hao kiasi cha kuhatarisha maisha yao na kudhoofisha shughuli za kiuchumi huku wakiipongeza TAWA kwa hatua yao ya kuwashirikisha wananchi katika zoezi zima la kukabiliana na changamoto hiyo.

"Kumekuwa na malalamiko makubwa sana kutokana na wimbi la wanyamapori hatarishi hususani fisi na wengine ambao wamekuwa wakishambulia watu, watoto wanashindwa hata kwenda shule, jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa" ameeleza Leonard Mayala mkazi wa Kahama

"Lakini ujio wa taasisi hii ya TAWA umekuwa ni faraja kubwa kwetu maana imekuja kwa ajili ya kushirikiana na wananchi ili kukabiliana na changamoto hii ya wanyamapori,..na mimi niseme, sisi kama wananchi tuko tayari kushirikiana na taasisi hii kwa sababu usalama ni wakwetu na taasisi hii imekuja na huu mpango kwa ajili ya kutuweka salama kwahiyo sisi wananchi tunaahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori hao" ameongeza

Naye Robert Wilson mkazi wa wilaya ya Misungwi Kata ya Mbarika ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikundi cha wagalu ameeleza kufurahishwa kwake na adhma ya Serikali kupitia TAWA ya kuwashirikisha wananchi katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika mapambano hayo ili jamii iwe na amani.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amewapongeza wananchi hao kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo na kusema kuwa ushirikiano huo unatoa mwelekeo mzuri katika kutatua changamoto inayowakabili wananchi hao.

Katika kusisitiza hilo, amesema kutokana na ukubwa wa nchi yetu na upungufu wa rasilimali ni dhahiri kuwa TAWA peke yake haitaweza kuwepo kila mahali, hivyo ushiriki wa wananchi katika uhifadhi na mapambano dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu ni muhimu katika kufikia malengo mapana ya uhifadhi wa wanyamapori nchini, hivyo TAWA inathamini maamuzi yaliyofanywa na wananchi hao.

Aidha ametoa rai kwa watanzania wote kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo ikizingatiwa kuwa jukumu la kulinda raia na mali zao ni la wananchi wote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com