WAPIGAKURA WAPYA 224,355 KUANDIKISHWA KIGOMA





Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma leo tarehe 29 Mei, 2024.



Na Mwandushi wetu, Kigoma
Wapiga kura wapya 224,355 wanatarajiwa kuandikishwa mkoani Kigoma wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika mkoani humo kwa siku saba kuanzia tarehe 01 hadi 07 Julai, 2024.

Uboreshaji huo wa Daftari utatanguliwa na uzinduzi wa zoezi hilo utakaofanyika tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma leo tarehe 29 Mei, 2024, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K amesema wapiga kura hao ni ongezeko la asilimia 21.50 ya wapiga kura 1,043,281 waliopo kwenye Daftari mkoani Kigoma.

“Kwa Mkoa wa Kigoma ambao una Halmashauri ya Manispaa moja, Halmashauri ya Mji moja na Halmashauri za Wilaya sita, majimbo ya uchaguzi nane na kata 488, Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 224,355. Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.50 ya wapiga kura 1,043,281 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hivyo, Tume inatarajia baada ya uandikishaji, Mkoa wa Kigoma utakuwa na wapiga kura 1,267,636,” amesema Bw. Kailima.

Akizungumzia makadirio ya wapiga kura wapya watakaoandikishwa nchi nzima, Bw. Kailima amesema Tume itaandikisha wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye Daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20.

“Katika zoezi hili, inatarajiwa wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 inatarajiwa wataondolewa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari. Hivyo, baada ya uboreshaji, inatarajiwa kuwa Daftari litakuwa na jumla ya wapiga 34,746,638,” amesema Bw. Kailima.

Kuhusu idadi ya vituo vya kuandikisha wapiga kura, Bw. Kailima amesema katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka huu wa 2024 kutakuwa na jumla ya vituo 40,126, ambapo kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar.

“Vituo hivi ni ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha wapiga kura mwaka 2019/2020,” amesema.

Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi amesema kwa Mkoa wa Kigoma vituo 1,162 vitatumika kwenye uboreshaji wa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 69 katika vituo 1,093 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Zoezi hili la uboreshaji litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 pamoja na wale ambao hawajapoteza sifa za kuendelea kuwemo kwenye Daftari kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyingine yeyote.

Uboreshaji pia utahusu kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa awali na ambao wamehama kutoka mkoa au wilaya moja kwenda nyingine waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali.

Zoezi hilo pia litatoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post