Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATAALAMU NGAZI ZA MIKOA NA HALMASHAURI WAHIMIZWA KUHAMASISHA UZALENDO KWA JAMII

 


Na WMJJWM- Dodoma

Wataalamu wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii na Kada nyingine kutoka ngazi ya Mikoa, Halmashauri na kata nchini wametakiwa kuhamasisha Jamii kuwa wazalendo, kujitolea na kuchangia katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Hayo yamesemwa Mei 22, 2024 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Patrick Golwike wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wataalam kutoka ngazi ya Mikoa na Halmashauri kuhusu utekelezaji wa Mpango wa kuhamasisha na kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa mwaka 2022/23-2025/26. 

Golwike amesema Serikali inatambua mchango wa Timu ya Wataalamu ngazi ya mkoa, wilaya na kata katika kutoa huduma kwenye nyanja mbalimbali kwa jamii kwa kuandaa mafunzo hayo yatakayowezesha Mpango huo kuwafikia wataalamu waliopo kwenye maeneo yao kwa haraka. 

"Natoa rai, kuwa ujuzi mtakaoupata mkautoe kwa Wataalamu wa ngazi ya kata ambao ndiyo kiungo muhimu baina ya Wananchi na Serikali" amesema Golwike 

Aidha, Golwike amewaagiza wataalamu hao kwa kila mkoa uandae na kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa Mpango kwa kuanza kutoa mafunzo ya Mpango kwa Wataalamu ngazi ya msingi kwani bila ya kuwa na mpango kazi wa utekelezaji ni upotezaji wa rasilimali fedha na muda, kuweka mpango wa utaratibu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi Ngazi ya msingi badala ya kusubiri viongozi wa ngazi za juu na kujenga mazoea ya kufanya kazi kwa timu na kuwajibika ili kuwa na kazi zenye matokeo na tija.

Pia ameagiza timu za Wataalamu ngazi ya Wilaya na kata kuwezeshwa ili kuhakikisha wanafanya vikao vya kufuatilia utekelezaji wa Mpango na kufanya maboresho kwenye maeneo yanayohitaji marekebisho na kuandaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji.

Vilevile amesema matokeo ya kuhamasisha uzalendo kwa jamii yatafanya kuwa na Taifa linalopenda yao, jamii inayofanya kwa bidii na jamii inayojitolea katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara za Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Jeremiah Mwambange amesema muamko wa wananchi kujitokeza katika shughuli za maendeleo kwa takwimu zilizopo ni asilimia 5 tu hivyo jitahada zaidi zinahitajika katika kuhamasisha wananchi kujitolea na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

"Suala la Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa Mwaka 2022/23 - 2025/26  ni la muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu kwani litasaisia kuamsha arinya wananchi kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika maeneo yao" amesema Mwambange

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Neema Ndoboka amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa Maafisa wa Serikali waliopo katika ngazi za Halmashauri na Mikoa ili waweze kuhakikisha Mpango huo unatekelezwa kikamilifu katika maeneo yao.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com