Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI NDEJEMBI ATEMBELEA OSHA, ASISITIZA UWEKEZAJI ZAIDI KATIKA TEHAMA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ) Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi wa Menejimenti ya OSHA wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za OSHA Dar es salaam kwa lengo la kuangalia mwenendo wa kiutendaji wa taasisi hiyo.

**************

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi amefanya ziara katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza jinsi Taasisi hiyo iliyopo chini ya Wizara yake inavyotekeleza majukumu yake.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni takribani mwezi mmoja baada ya Kiongozi huyo kuteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo ya kusimamia Masuala ya Kazi na Ajira nchini kutokana na mabadiliko madogo yaliyofanyika katika Baraza la Mawaziri Machi 31, 2024.

Akizungumza na Menejimenti ya OSHA mara baada ya kusikiliza wasilisho la Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, kuhusu OSHA na majukumu yake, Waziri Ndejembi ameitaka menejimenti ya OSHA kuwekeza zaidi katika mifumo kidijitali ili kurahisisha utendaji na kuongeza ufanisi.

Kadhalika, ameiagiza OSHA kuongeza jitihada katika kuwaelimisha na kuwahamasisha wadau wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi ili waweze kutekeleza sheria na miongozo mbali mbali ya usalama na afya kwa hiari.

“Sina mambo mengi kwa siku ya leo kwani nimekuja kwa lengo la kujifunza kuhusu utendaji wenu mkiwa miongoni mwa Taasisi chini ya Wizara ninayoiongoza ili kwa pamoja tuweze kushirikiana kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu. Nimejifunza mengi kutokana na wasilisho la Mtendaji Mkuu hivyo ninawashauri kuwekeza zaidi katika mifumo ya TEHAMA pamoja na kubuni mikakati ya kuongeza uelewa miongoni mwa wadau wenu na wananchi kwa ujumla ambao uelewa wao kuhusu masuala haya bado ni mdogo,” ameeleza Waziri Ndejembi.

Aidha, Ndejembi ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Mashirikiano (Memorandum of Understanding) baina ya OSHA na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) yatakayoziwezesha Taasisi hizo mbili kushirikiana katika mambo mbali mbali hususan suala la utoaji elimu ya usalama na afya kwa wanachama wa TUGHE nchini.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, pamoja na kuwasilisha mada kuhusu utendaji wa OSHA katika kikao hicho, amempongeza Waziri Ndejembi kwa kuteuliwa kuiongoza Wizara ya Kazi na Ajira ambapo amemuahidi Waziri kuhakikisha kwamba Taasisi ya OSHA inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kututembelea ambapo tumepata fursa ya kumpitisha katika majukumu yetu nae ametushirikisha maono yake kuhusiana na sekta hii ya Kazi na Ajira hususan eneo hili mtambuka la usalama na afya mahali pa kazi ambalo linagusa kila sekta. Hivyo, tunamuahidi yeye (Mhe. Waziri) pamoja na Mheshimiwa Rais aliyemteua kuwa tutafanya kazi kwa bidii katika kufanikisha maono ya viongozi wetu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Katibu Mkuu wa TUGHE, Bw. Hery Mkunda, amesema makubaliano waliyofanya na OSHA yanalenga kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanapatiwa haki yao ya msingi ya kulindwa kutokana na vihatarishi mbali mbali mahali pa kazi.

“Kwa mujibu wa Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambayo nchi yetu imekubaliana nayo, masuala ya usalama na afya yamekuwa ni haki ya msingi ya wafanyakazi hivyo sisi kama TUGHE tumeona ni muhimu tukafanya kazi kwa karibu na OSHA ili kuhakikisha kwamba haki hiyo inapatikana,” ameeleza Comrade Mkunda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ) Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi wa Menejimenti ya OSHA wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za OSHA Dar es salaam kwa lengo la kuangalia mwenendo wa kiutendaji wa taasisi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akiwasilisha mada juu ya mwenendo wa taasisi ya OSHA mbele ya Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Deogratius Ndejembi Pamoja na viongozi wa menejiment ya OSHA wakati wa kikao kifupi na Waziri huyo.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (kulia) na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Comrade. Hery Mkunda (kushoto) wakisaini hati ya Makubaliano baina ya OSHA na TUGHE ya mashirikiano ya kutoa elimu ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi nchini mbele ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ) Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhi Hati ya Makubaliano ya Mashirikiano kati ya OSHA na TUGHE ya kutoa elimu ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi wa sekta mbalimbali nchini kwa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ) Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhi Hati ya Makubaliano ya Mashirikiano kati ya OSHA na TUGHE ya kutoa elimu ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi wa sekta mbalimbali nchini kwa Katibu Mkuu wa TUGHE, Comrade. Hery Mkunda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com