WIKI YA AZAKI 2024 YAZINDULIWA RASMI JIJINI DAR

DAR ES SALAAM - MEI 21,2024

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society (FCS) Justice Rutenge, amesema katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050 wananchi wanapaswa kupaza sauti zao kwa kutoa maoni yatakayopelekea kupata Dira bora kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Rutenge ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2024, itakayofanyika Septemba 9 hadi 13 Jijini Arusha ambapo zaidi ya washiriki 500 wanatarajiwa kushiriki.

Ameeleza kuwa maadhimisho hayo mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo 'Sauti, Maono na Thamani' lengo likiwa ni kutoa fursa zaidi kwa wananchi kupaza sauti zao kwa pamoja ili kurahisisha mchakato mzima wa upatikanaji wa Dira hiyo.

"Kaulimbiu ya Wiki ya AZAKI mwaka huu, inalenga kuwa na Dira nzuri licha ya tofauti ya mitazamo ya watu na makundi, bado sauti zetu zinapaswa kuwa kitu kimoja ili kurahisisha mchakato wa Dira ya maendeleo ya Taifa 2050" amesema Rutenge.

Aidha, amesema FCS inajukumu kubwa la kuziwezesha Asasi za Kiraia kushiriki kwenye maendeleo ya watu, na kwamba Wiki ya AZAKI itajumuisha Asasi mbalimbali zitakazoshiriki maadhimisho hayo.

Ameongeza kuwa, Wiki ya AZAKi mwaka huu inafanyika mapema mwezi Septemba, tofauti na ilivyozoeleka ambapo hufanyika mwezi Oktoba tangu kuanzishwa kwake 2018, nakwamba lengo la mabadiliko hayo ni kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwezi Octoba mwaka huu.

Wiki ya AZAKI mwaka huu imefadhiliwa na Vodacom Foundation na wadau wengine wa maendeleo, zikiwemo Asasi za Kiraia, ambapo katika Wiki hiyo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo njia zinazoweza kuleta thamani halisi na chanya kwa kufikia maono ya pamoja ya mustakabali wa nchi na kuimarisha ushirikiano baina ya Sekta Binafsi, Umma, na Asasi za kiraia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post