Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola, (kulia) akikabidhi kishikwambi kwa Mjumbe wa Bodi. Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 28/6/2024 katika ukumbi wa SHUWASA Ofisi Kuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingiara Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola, (kushoto) akikabidhi kishikwambi kwa Mwenyekiti wa Bodi, Bi. Mwamvua Jilumbi. Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 28/6/2024 katika ukumbi wa SHUWASA Ofisi Kuu.
NA MWANDISHI WETU, SHINYANGA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imegawa vishikwambi kwa wajumbe 10 wa Bodi ya Wakurugenzi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Akizungumza mara baada ya kugawa vishikwambi hivyo leo tarehe 28/6/2024, Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia karatasi lakini hivi sasa wamehamia kwenye vishikwambi ili kuendana na teknolojia.
Ameeleza kuwa matumizi ya vishikwambi yataongeza ufanisi kwani vitarahisisha maandalizi ya vikao kwa kutoa mapema taarifa za utendaji kazi na mihutasari kwa Wajumbe wa Bodi ili waweze kuanisha maeneo muhimu ya kujadili wakati wa vikao.
“Katika uandaji wa vikao vya Bodi taarifa za utekelezaji wa vitengo pamoja na muhtasari zimekuwa zikiandaliwa kwenye karatasi, lakini tumeona sasa tubadilike twende na teknolojia tuachane na makaratasi,” amesema Mhandisi Yusuph.
“Kuanzia robo ya kwanza yam waka 2024/2025 vikao vya bodi havitakuwa tena na karatasi badala yake itakuwa vishikwambi,” ameongeza.
Aidha amesema, Mamlaka hiyo haitaishia kwa wajumbe wa bodi na badala yake hata wajumbe wa menejimenti ya SHUWASA nao watapatiwa vishikwambi ili kuondoa kabisa matumizi ya karatasi.
Ameeleza mbali na kuongeza ufanisi, matumizi ya vishikwambi yatapunguza gharama za uendeshaji wa Mamlaka kwa kuepuka gharama za uchapishaji wa karatasi.
Naye Mjumbe wa Bodi anayeiwakilisha Wizara ya Maji, Bw. Nicholaus Nyumbo ameipongeza menejimenti ya SHUWASA kwa kuleta mabadiliko hayo ambayo yataongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Bodi.
“Vishikwambi hivi vitaturahisishia kupata taarifa mapema ili tuweze kujiandaa na vikao tofauti na ilivyokuwa sasa ambapo ilibidi kila mjumbe atafutwe alipo apewe kabrasha ambayo ni mengi. Kwahiyo tumepunguziwa pia mzigo wa kubeba karatasi,” amesema