Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI, WADAU WAASWA KUENEZA ELIMU KATIKA JAMII KUHUSU HUDUMA ZA TIBA KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA


 

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Uraibu wa dawa za kulevya ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine. Waraibu ni wagonjwa na siyo wahalifu! Ni kauli kutoka kwa baadhi ya waliokuwa watumiaji wa dawa za kulevya lakini sasa wameachana na utumiaji wa dawa hizo na kurejea katika hali zao za awali.

Wakati Dunia ikiadhimisha Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya mwaka 2024, yapo mafanikio ya kujivunia kupitia afua ya huduma kwa waraibu (MAT) inayotolewa katika mikoa ya Pwani na Tanga kupitia mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika la THPS kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (US. CDC).
Mariam Semwaza ni mmoja wa wanufaika wa huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya kupitia kituo cha huduma za MAT kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo kinachowezeshwa na THPS kwa kushirikiana na Serikali, anasema kituo hicho kimemsaidia kwa kiasi kikubwa kumbadilisha tabia baada ya kuwa mraibu wa dawa za kulevya kwa zaidi ya miaka 15.

Mariam (50) ameeleza kuwa katika kipindi hicho alikuwa mtumiaji wa Bangi, Heroine na Pombe lakini ameachana na matumizi ya dawa hizo na sasa amejiunga katika program ya tiba ya Methadone katika kituo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya mkoani Tanga na anajutia utumiaji wa dawa za kulevya kwani ulimwathiri Kisaikolojia, Kimwili na Kiuchumi.

“Nilishawishiwa kuanza kutumia dawa za kulevya na rafiki yangu ambaye alikuwa ananinunulia pombe na sigara bila ya mimi kujua kuwa alikuwa ananichanganyia na dawa za kulevya. Hali hii ilipelekea nikawa teja wa kutafuta dawa za kulevya mtaani nikilazimika kujiunga na magenge ya wizi, ambapo tulikuwa tunaiba ili tupate pesa za kununulia dawa za kulevya. Nikawa sithamini nyumbani hadi mume wangu akaamua kuniacha. Nilipata mateso makubwa ya kupigwa, kukamatwa na askari”,anasimulia Mariam.

“Kutokana na mateso niliyopata, ikiwemo kufungwa gerezani, nikafikia maamuzi ya kujiunga na huduma ya MAT licha ya kukatishwa tamaa na baadhi ya waraibu wenzangu waliokuwa wanasema dawa ya Methadone inaua. Baada ya kuanza tiba niliweza kuacha kabisa kutumia dawa za kulevya, naendelea kutumia Methadone, sijavuta bangi, heroine wala kunywa pombe na najishughulisha na ushonaji nguo na utengenezaji Batiki ili kujipatia kipato”,ameongeza Mariam.
Mariam Michael Semwaza akiwa katika viwanja vya Nyamagana Jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga vita dawa za kulevya duniani 2024

Amezitaja sababu zinazochangia watu kuingia katika wimbi la utumiaji wa dawa za kulevya kuwa ni ushawishi wa marafiki, kusingizia msongo wa mawazo na unywaji pombe uliokithiri hali hali inasababisha mtu kuharibikiwa na kuwa mraibu wa dawa za kulevya.

Ameitaka jamii kuwaelimisha waraibu wa dawa za kulevya umuhimu wa kujiunga kwenye huduma za tiba badala ya kuwanyanyapaa na kuona ni wahalifu.

“Waelimisheni waraibu wa dawa za kulevya kuhusu huduma za MAT. Inawezekana kabisa wakabadili tabia zao, mfano mimi nimetumia dawa za kulevya kwa miaka mingi, nilikuwa sijitambui lakini sasa nimerejea kwenye hali yangu ya awali”, amesema Mariam.

“Na msiwabague wala kuwanyanyapaa waraibu wa dawa za kulevya walioanza kupata huduma za Tiba, hao wameamua kubadilika, wameachana na hayo mambo ya dawa za kulevya, msiseme ni wale wale”,amesisitiza Mariam.


Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (Medically Assisted Therapy – MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo Dkt. Wallace Karata amesema wanashirikiana na asasi mbalimbali huku akiitaka jamii kuwapeleka waraibu wa dawa za kulevya kwenye vituo ili waanzishiwe tiba ili kukabiliana na wimbi uraibu ambao pia unachangia maambukizi ya VVU.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo Dkt. Wallace Karata akielezea namna wanavyotoa huduma kwa waraibu wa dawa za kulevya

“Katika kituo cha MAT cha Tanga tangu tumeanza kutoa huduma mwaka 2020 hadi hadi sasa tumesajili waraibu wa dawa za kulevya 1,129 kati yao wanawake ni 31, wanaume 1,098. Kati ya hao waliohitimu katika programu ya Methadone ni 72. Kila siku tunapokea wateja takribani watatu lakini changamoto ni kwamba baadhi yao wanaachia njiani hawafiki mwisho”,amesema Dkt. Wallace.


“Kati ya hao waraibu wa dawa za kulevya 687 pekee ndio wanaendelea kutumia dawa za Methadone. Waraibu 445 wamepotea katika huduma, 67 wanaishi na maambukizi ya VVU, 7 waliofungwa jela”,ameongeza Dkt. Wallace.

Amebainisha kuwa, kituo cha MAT cha Tanga kimekuwa kikipokea waraibu wa dawa za kulevya kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar, Mombasa na Nairobi nchini Kenya na kwamba idadi yao imekuwa ikiongezeka kila siku.

“Natoa wito kwa jamii tuwachukulie waraibu wa dawa za kulevya kama wagonjwa siyo wahalifu, tusiwaone kama wahalifu na naomba wale ambao hawajaanza kupata huduma ya tiba waletwe kwenye taasisi hizi za serikali zilizopo katika Hospitali za Rufaa mfano Tanga kwani sisi tuna dawa nyingi na tunao wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha waraibu wa dawa za kulevya wanabadilika tabia licha ya kwamba mabadiliko ya tabia ni jambo linalochukuwa muda mrefu”,ameeleza Dkt. Wallace.


Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Tanga, Imani Clemence Rwatamabanga anaupongeza mradi wa Afya Hatua kwa uwekezaji mkubwa ilioufanya kwenye kituo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ambapo waraibu wa dawa za kulevya wanaendelea kupata huduma za tiba ili warejee kwenye hali zao za awali.
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Tanga, Imani Clemence Rwatamabanga.

“Shughuli za THPS mkoani Tanga zinaenda vizuri kwa kushirikiana na serikali mmeweka nguvu kubwa sana pale kwenye kituo cha MAT. Tunao watu wenye uhitaji wa huduma za tiba, vyombo vya habari tangazeni mambo makubwa yanayofanyika MAT ili watu wenye uhitaji wa tiba waje zaidi, huduma ni nzuri sana na waraibu wa dawa za kulevya wanazidi kupata huduma”,ameongeza Rwatamabanga.

Afisa Ustawi wa Jamii Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga, anayehudumia waraibu, Bertha Mbaruku ameiomba serikali itilie mkazo kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya na biashara ya dawa za kulevya kuanzia ngazi za chini mfano shuleni, vikao na mikutano mbalimbali kwa sababu kinga ni bora zaidi kuliko tiba kwani gharama za kutibu waraibu wa dawa za kulevya ni kubwa.


“Dawa za kulevya zina madhara mengi kwani zinagharimu afya na ustawi wa mtumiaji wa dawa hizo, zinasababisha kifo, uhalifu na waathirika wa dawa hizo kutengwa, kuathirika kisaikolojia, hofu kwenye familia zenye watumiaji wa dawa hizo. Hivyo ni vyema elimu zaidi iendelee kutolewa kuanzia ngazi za chini kabisa ili watoto wakue wakijua madhara yatokanayo na dawa za kulevya lakini pia Serikali iongeze nguvu zaidi katika kudhibiti njia za uingizaji dawa za kulevya”,amesema Bertha.

Kwa upande wake, Afisa Utawala wa asasi ya Gift of Hope Foundation ambayo kupitia mradi wa Afya Hatua inafanya kazi ya kuwatambua waraibu, kuwapatia elimu na kuwaunganisha na huduma za MAT, Abubakar Kassim Zuberi amesema waraibu wa dawa za kulevya wana ujuzi mbalimbali hivyo ameishukuru Serikali na wadau mbalimbali kwa kuendelea kuwawezesha kiuchumi ikiwemo kuwapatia ruzuku na Mashine za kufyatulia matofali, kunyolea na cherehani kupitia vikundi vitano vyenye wanachama 50 mkoani Tanga.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo Dkt. Wallace Karata akielezea namna wanavyotoa huduma kwa waraibu wa dawa za kulevya
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo Dkt. Wallace Karata akionesha mabadiliko ya waliokuwa waraibu wa dawa za kulevya hali ya sasa na kabla
Muonekano wa picha za kabla na baada ya kuacha kutumia dawa za kulevya
Mmoja wa wanufaika wa huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya kupitia kituo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (Medically Assisted Therapy – MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, bi. Mariam Michael Semwaza akielezea namna alivyofanikiwa kujinasua katika uraibu wa dawa za kulevya
Mtaalamu katika kituo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (Medically Assisted Therapy – MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga akielezea namna wanavyotoa huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (Medically Assisted Therapy – MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo Dkt. Wallace Karata akielezea namna wanavyotoa huduma kwa waraibu wa dawa za kulevya
Viongozi wa THPS (kushoto) wakifanya mazungumzo na Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Tanga, Imani Clemence Rwatamabanga.

Mmoja wa wanufaika wa huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya kupitia kituo cha Huduma za Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (Medically Assisted Therapy – MAT) kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, bi. Mariam Michael Semwaza akiwa katika viwanja vya Nyamagana Jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga vita dawa za kulevya duniani 2024

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com