Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewakaribisha watanzania hususani wakazi wa mkoa wa Mwanza na maeneo jirani kujitokeza katika maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya ambapo kitaifa yanafanyika mkoani humo June 30 mwaka huu katika viwanja vya Nyamagana huku mgeni rasmi wa maadhimisho hayo akitarajiwa kuwa Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo mapema leo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza na kusema kwamba maadhimisho hayo yatafunguliwa na kuanza June 28 katika viwanja vya Nyamagana ambapo katika viwanaja hivyo wananchi watapata fursa ya kupewa elimu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya .
‘’Malengo ya kuuadhimisha siku hii ni mengi lakini niseme machache maadhimisho haya yatatoa fursa kwa wananchi kupata elimu ya athari za matumizi,pia mtu alietumia madawa hayo ataathirika kisaikolojia na kiuchumi pia,Watanzania lazima wajue jitihada za serikali katika kupambana na dawa hizi hivyo ni fursa kwa watanzania kupata elimu hii”, amesema Mtanda
Aidha Mhe. Mtanda amesema pamoja na Uzinduzi huo wa maadhmiisho hayo ambao utafanyika June 28 katika viwanja vya Nyamagana pia kutakuwa na kongamano maalumu la kitaifa juu ya tatizo la dawa za kulevya ambalo litafanyika katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali.
Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ni “Wekeza kwenye kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya”