TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YATOA ELIMU YA KUHUSU HAKI ZA BINADAMU BUKOBA


Kamishna wa Tume ya haki za binadamu na utawala bora  Nyanda Shuli akizungumza 
Diwani wa Kata ya Bilele Mh Sharif Salum Taufiq akizungumza 

Na Mbuke Shilagi Kagera

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imefanya ziara ya siku mbili Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera lengo ikiwa ni kutoa elimu juu ya haki za binadamu kwa wananchi na wakazi wa manispaa ya Bukoba.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika soko kuu la Bukoba lililopo ndani ya Kata ya Bilele Juni 11, 2024, Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora Mh. Nyanda Shuli amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora ni idara inayojitegemea ya Serikali na ni chombo cha Nchi kinachofanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar.

"Chombo hiki kimeundwa kwa mujibu wa katiba ili kusaidia na kuwezesha utetezi ufatiliaji na ulinzi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora", amesema Kamishina Shuli.

"Kwahiyo bahati nzuri sana utawala bora katika nchi yetu umewekwa katika ngazi tofauti tofauti na tume hii pamoja na kuwepo mahakama na ofisi mbalimbali za Serikali kuhudumia wananchi lakini ilionekana ni vyema kuwepo na hiki chombo ili mwananchi anapokosa msaada na kuona anashindwa kupata haki zake katika maeneo mengine aje tume na anapofika tume sisi tumepewa nguvu na katiba na sheria ya kwenda popote pale ambapo kunamkwamo'' ,amesema.

Naye Afisa uchunguzi Mkuu kutokavTume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Konstantine Mugusi amesema kuwa haki za binadamu ni zile haki au stahili ambazo mtu anasitahili kuzidai kwasababu yeye ni binadamu.

"Ubinadamu wako unakufanya ustahili haki ambazo dunia imezitambua na kuziainisha katika sheria za kimataifa,za kikanda na hata katika katiba yetu ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

"Haki anayositahili Mtanzania ndiyo haki anayo sitahili Mmarekani na hizi haki zinategemeana na ukinyang'anya haki moja kuna uwezekano wa kunyanganya haki kadhaa na hizi haki hazitenganishwi na huwezi kuzirithisha kwahiyo ukomo wa kuzisitahili ni urefu wa maisha yako"

"Serikali ndiyo yenye jukumu la kuzilinda lakini serikali hiyo imewekewa mamlaka nyingine ili kuona kweli inazilinda? mfano bwana serikali ulisema utalinda haki ya elimu ulisema utailinda haki ya kumiliki mali unailinda? mbona huilindi yenyewe kama ulivyosema?",amesema.

Aidha katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ngazi ya Wilaya,Kata,Mitaa pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa Bukoba wamepata nafasi ya kuwasilisha malalamiko yao ambayo yamekuwa mzigo kwako.

Ambapo mwananchi ambaye amejitambulisha kwa jina la mchungaji William Polotas Bashange amelilalamikia jeshi la Polisi Bukoba kwamba limeshindwa kumsaidia na kuwa usumbufu katika familia yake baada ya mtu mmoja kutoka Jeshi la Polisi alistaafu na kuwa msumbufu katika familia yake.

"Jeshi la Polisi sijui wamekaa sana hapa na kuzoea mazingira haya? ni watesaji naomba tume iende jeshi la polisi inisaidie" amesema Mch. Bashange.

Naye Kamishina  wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Nyanda Shuli amejibu na kusema kuwa tume ya haki za binadamu na utawala bora miongoni ya majukumu yake ni wananchi wanapata huduma bora huku akisema kuwa amani ni zao la haki na mahali ambapo hapana haki uwezi kupata amani.


"Mzee Bashange tunaendelea kuchukua maelezo yake vizuri ili tuone jambo lake tunalifuatilia vizuri na sisi tunapochukua maelezo hatukai upande wa mlalamikaji au mlalamikiwa ila tunasimama upande wa haki na ndiyo majukumu ya tume hii", amesema.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bilele Mh. Shariff Salum Taufiq ameiomba serikali pamoja na wizara ya tume ya haki za binadamu na utawala bora kuweka ofisi katika Mkoa wa Kagera ili wananchi kupata sehemu ya kukimbilia kuliko ilivyo hivi sasa ambapo ofisi ipo Mwanza.

"Ushauri wangu ni kwamba katika vikao vyenu nchii hii ni kubwa hivyo kila mkoa ziwepo ofisi angalau hata mtu wa ngara anaweza kuja hapahapa ndani ya mkoa na kutoa malalamiko yake na akapata haki yake", amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post