DC SIIMA : UJIO WA MADAKTARI BINGWA KUONDOA CHANGAMOTO KWA WANANCHI KAGERA

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh. Erasto Siima akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera  katika hospitali ya Wilaya ya Bukoba Nshambya katika uzinduzi wa kambi ya madaktari bingwa. 

Na Mbuke Shilagi Kagera. 

Mkuu wa wilaya ya Bukoba amesema kuwa Ujio wa madaktari bingwa katika Mkoa wa Kagera unaenda kusaidia kuondoa changamoto kwa wananchi kufuata huduma za kibingwa nje ya mkoa wa Kagera na kupunguza umbali mrefu pamoja na gharama.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh. Erasto Siima  amesema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera  June 17,2024 katika hospitali ya Wilaya ya Bukoba Nshambya katika uzinduzi wa kambi ya madaktari bingwa wa magonjwa ya usingizi, mama na mtoto, upasuaji mkubwa pamoja na magonjwa ya ndani. 

Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha zaidi huduma za afya kwa maslahi ya watanzania huku akisema asilimia 85.2 imehudumia jamii ya mama na mtoto kwa mwaka 2024.

Hata hivyo ameongeza kuwa huduma za afya ya mama na mtoto imezidi kuimarika na kuongezeka zaidi na kuondoa changamoto iliyokuwepo kwani huduma hii itaondoa changamoto ya wananchi kwenda nje ya mkoa.

"Nipende kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na nimshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan japokuwa na kazi na ratiba nyingine alizonazo lakini suala zima la afya zetu halipo nyuma katika majukumu yake ya kila siku kwamaana madakitari wote waliopo hapa leo ni kwamatakwa yake",amesema Dc Siima.

Kwa upande wake afisa idara ya afya ya uzazi mama na mtoto bi Grace malick ambae ameongozana na madaktari bingwa kutoka wizara ya afya nchini amesema lengo la kambi hiyo ni kuhakikisha huduma za kibingwa zinawafikia wananchi wote na kupata huduma hizo kwa bei nafuu na kupunguza umbali kwa wananchi wanaotoka maeneo ya mbali.

Ameongeza kuwa Huduma hiyo ya mama Samia Mentorship inatekelezwa katika mikoa yote 26 na sasa mikoa 23 tayari ishapata huduma hii  na halmashauri  139 kati ya halmashauri 184 na  ipo katika mkoa wa Kagera tayari kwa huduma hiyo katika halmashauri zote 8.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Mh. Jakob Nkwera amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia kwa kusogeza huduma ya kibingwa katika ngazi ya chini ili kuwafikia watu wote bila ya kuingia gharama kubwa. 

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba ameshukuru kwa ujio wa madaktari hao na kuwataka wananchi ndani ya Manispaa ya Bukoba kuhakikisha wanafika katika kata ya nshambya na hospitali ya Nshambya ili kuweza kujipatia huduma hizo za kibingwa ambapo yameanza jumatatu June 17,2024 mpaka Ijumaa June 21,2024.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post