Na Mtemi Sona
Ukizungumzia sanaa ya ngoma za asili kanda ya ziwa, huwezi kuacha kumtaja mwana dada Martina Thomas. Kama wewe ni Mtazamaji, Martina akiwa jukwaani huwezi kuchoka kutazama jinsi anavyolishambulia jukwaa kwa uchezaji wake mahiri na wenye kuvutia. Ni dada ambaye ameteka hisia za wapenzi wengi wa ngoma hizo hasa wazungu kutoka mataifa ya Denmark na Sweden ambao hutembelea makumbusho ya Bujora kujifunza Utamaduni wa wasukuma.
Ukifika nyumbani kwake Kisesa Mwanza, utakuta chumba kikubwa ambacho amekigeuza kama sehemu ya kuhifadhia ngoma. Ukiingia ndani utaona ngoma za aina mbalimbali zimehifadhiwa sambamba zana tofauti za kuchezea ngoma hizo, zikiwemo nguo, simbi na vinyago. Martina ni mama wa watoto wanne, msichana mmoja na wavulana watatu, binti yake ambaye ndiye mtoto wake wa kwanza anaitwa Regina, wapo wanaomuita mama Regina na wengine hupenda kumwita Martina.
Kwa zaidi ya miaka 30, Martina Thomas Lubango, amekuwa msanii wa ngoma za asili za kabila la Wasukuma, akifundisha kuimba na kucheza ngoma hizo watu wa mataifa mbalimbali wakiwemo wazungu kutoka nchi za Sikadinavia hususani Denmark na Sweden. Anafundisha kuimba na kucheza kwa kutumia Wanyama kama vile nyoka. Amesaidia kufundisha vikundi vya ngoma za asili za kabila la wasukuma vilivyoanzishwa katika nchi za Denmark na Sweden kupitia tamasha kubwa la Utamaduni ambalo hifanyika kila mwaka chini Denmark.
Martina Thomas Mnde Lupango, ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya Baba Thomas Lubango na mama Flora Mashimba, anaishi katika mji wa Kisesa Mwanza. Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, shule ya msingi Bujora 1995, alianza kujihusisha na sanaa ya uchezaji ngoma za asili. Safari hiyo ya sanaa aliianza muda mrefu tangu akiwa bado anasoma shule ya msingi Bujora, alishiriki michezo mbalimbali ikiwemo ngoma, maigizo na sarakasi. Mama yake mzazi alikuwa pia msanii wa kikundi cha Sanaa cha Kiwanda cha nguo Mwanza “Mwatex”, na wajomba zake walikuwa ni wasanii pia ambao baadaye walikuja kumfundisha kucheza mchezo wa sarakasi. Kupitia kushiriki michezo mbalimbali shuleni na wakati mwingine Kanisani, Padre Alexander Machunda Mugonya ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bujora alimuona na kugundua kipaji chake, hivyo alimchukua na kumuingiza katika Kikundi cha vijana wana wito wa Kanisani ambapo ndipo kipaji chake kilizidi kukua zaidi. Alishiriki michezo mingi Kanisani hapo sambamba na watoto wenzake.
Kufuatia jitihada za Padre Mugonya, mwaka 1996, walichaguliwa Watoto 12 kwenda nchini Denmark kuonyesha michezo ya ngoma na sarakasi na yeye akiwa ni miongoni mwa Watoto hao. Akiwa nchini Denmark alionyesha uwezo mkubwa wa kucheza sarakasi hali iliyowavutia sana wazungu. Baada ya kurudi kutoka Denmark, Martina alijiunga na kundi la Sanaa la Wana Sesilia ambalo lipo chini ya Makumbusho ya Kabila la Wasukuma Bujora “Sukuma Museum” akawa sehemu ya kundi hilo.
Kupitia Kundi la wana Sesilia, nyota ya Sanaa ya Martina ilizidi kung’ara zaidi na kuwa kivutio kwa watalii wengi waliokuwa wanatembelea Makumbusho hayo. Pamoja na kuanza kwa kucheza ngoma ya Banungule ambayo sifa yake kubwa ni kucheza na wanyama kama vile fisi na Nungunungu, pia aliweza kucheza ngoma zingine zaidi za kisukuma ambazo ni Bogobogobo, Sogota, Pachanga, Buzwiriri, Bulabuka na Buyeye.
Safari za Kwenda Ulaya kama Msanii na mwalimu wa ngoma, zilianza rasmi mwaka 2002, ambapo baadhi ya wazungu waliomuona wakati walipotembelea Tanzania na kuvutiwa na kipaji chake na kutamani kujifunza ngoma hizo, walimualika kwenda nchini Denmark kwa lengo la kuwafundisha utamaduni huo. Akiwa nchini Denmark, alishiriki Tamasha kubwa la Utamaduni ambalo hufanyika kila mwaka katika mji wa Ramten skov, tamasha hilo linahusisha Utamadani wa Afrika hususani ngoma za Kisukuma
Maisha ya Martina katika Kundi la Wanasesilia yalikuwa ya kupendeza yaliyopambwa na kila aina ya burudani, hasa matamasha ambayo kundi hilo lilikuwa likishiriki. Alijitoa katika kundi hilo na kuanzisha kundi lake ambalo alilipa jina la Buyegu lengo likiwa kuzidi kuutangaza zaidi utamaduni wa Kitanzania kwa mataifa mengine.
Safari za ulaya zimemuwezesha kupata kipato, ameweza kujenga nyumba na kusomesha watoto. Pia anaendelea kupokea wageni kutoka mataifa ya Denmark na Sweden ambao wanakuja kujifunza kucheza ngoma. Richard Buluma, ambaye ni mhifadhi katika makumbusho ya Bujora, anamuelezea Martina kama dada mwenye uwezo mkubwa katika kufundisha ngoma hizo, wageni hasa wazungu wamekuwa wakipenda kujifunza hizo ngoma.
Kupitia Sanaa, Martina amefanikiwa kujiajiri na kutoa ajira kwa vijana wengine wa Kitanzania. Kundi lake la Buyegu limekuwa likipata mialiko ya kushiriki matamasha mabalimbali likiwemo lile la Bulabo ambalo hufanyika kila mwaka katika Mji wa Kisesa.
Pamoja na sanaa, Martina pia anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga (Hotculture. Anatoa wito kwa jamii kuwa wazalendo kwa kupenda vitu vya kwao na kuenzi utamaduni akinukuu kauli ya Baba wa taifa Julius Nyerere aliyewahi kusema “Taifa ambalo halina Utamaduni ni sawa na Taifa mfu”.
Anashukuru na kupongeza Serikali kwa mchango inaotoa katika Sanaa. Anaomba wadau wengine yakiwemo mashirika na taasisi mbalimbali binafsi na zile za Serikali kuendelea kuwashika mkono wasanii wa ngoma za asili kwa kuwapa kazi lakini pia kuboresha masilahi yao kwa kuwalipa vizuri kama wasanii wengine ili nao waweze kukidhi mahitaji yao. Anawashauri wasanii wenzake wa ngoma za asili kushirikiana na kufanya kazi pamoja kwa lengo la kutangaza zaidi Utamaduni wa Tanzania.
Social Plugin