Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGEJA AKERWA MPINA KUFUKUA MAKABURI, ATAKA RAIS SAMIA ATANGAZE MIWA ZAO LA KIMKAKATI


Khamis Mgeja

MMOJA wa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan alitangaze zao la miwa inayotengeneza sukari kuwa moja ya mazao ya kimkakati hapa nchini.

 Mgeja ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga na sasa ni mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation yenye makao yake wilayani Kahama amesema iwapo zao la miwa ya sukari litapewa kipaumbele litamaliza changamoto ya uhaba wa sukari hapa nchini. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini Kahama kada huyo maarufu wa CCM alisema mbali ya Rais Samia kulitangaza zao la miwa kuwa zao la kimkakati lakini pia Serikali yake iwahamasishe watanzania wenye uwezo kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya sukari hapa nchini.


 Alisema iwapo watanzania wengi watajenga viwanda vya sukari ikiwemo vile vikubwa, vya kati na vidogo vidogo ni wazi changamoto ya uhaba wa sukari hapa nchini itamalizika na Tanzania itaweza kuuza sukari nchi za nje tofauti na hali ilivyo hivi sasa.


 “Binafsi mimi sifurahishwi na haya malumbano yanayoendelea hivi sasa hapa nchini kwetu ambayo yamesababishwa na changamoto ya uhaba wa sukari kuadimika kipindi fulani, kiasi cha baadhi ya wanasiasa kuibeba agenda hii na kuifanya mtaji wa kisiasa,”


 “Tiba ya changamoto hii ni kumuomba Rais Samia sasa atangaze kwamba kilimo cha miwa inayotengeneza sukari kipewe kipaumbele, watu walime miwa mingi, na zao hili liwe la kimkakati, naamini baada ya kipindi kifupi uhaba wa sukari hapa nchini utabaki kuwa historia, na tutaweza kuuza hata nje ya nchi,” alieleza Mgeja. 


Hata hivyo Mgeja aliendelea kueleza kuwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza hapa nchini zinapaswa kupatiwa utatuzi kwa watanzania wenyewe kushauriana na kupendekeza njia sahihi za kuzimaliza badala ya kuzigeuza mtaji wa kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa kuwachafua wenzao walioko madarakani. 


“Haya malumbano ya uhaba wa sukari hayajaanza leo, hata kipindi cha serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa yalijitokeza, sasa tatizo hili limekuwa likijirudia rudia nafikiri utatuzi wake ni kuzalisha sukari ya kutosha hapa nchini, na wanasiasa waache kulifanya mtaji wa kisiasa,”


 “Tumesikia wenyewe hivi karibuni sakata ambalo limetokea kule bungeni, ndugu yetu Luhaga Mpina ameibua hoja ya kumlaumu waziri Bashe akimtuhumu kulidanganya bunge kuhusiana na suala la vibali vya sukari, mbali ya kutoa hoja hiyo bungeni lakini alitoka nje na kuongea na vyombo vya habari, ikaleta shida,” alieleza Mgeja.


 Alisema yapo mambo ambayo yamewahi kufanyika hapa nchini bila kufuata utaratibu wa kisheria lakini kwa nia njema ya kukabiliana na changamoto iliyojitokeza kwa wakati huo lengo ikiwa ni kuwasaidia watanzania na watu walikaa kimya hawakulaumu wala kumshutumu kiongozi ye yote.


 Mgeja alifafanunua kuwa alichopaswa kufanya Mpina ilikuwa ni kukaa na Serikali na kuonesha mapungufu ambayo yeye anaamini ni mapungufu na kushauri nini kifanyike badala ya kulalamika na kumlaumu waziri mwenye dhamana na wizara ya kilimo kwamba amefanya makosa. 


“Nimuombe kijana wangu ambaye kwa kweli nimemkuza mimi mwenyewe kisiasa, Mheshimiwa Mpina, namuheshimu sana, lakini hanifurahishi hata kidogo kuona kila saa anafukua makaburi  badala ya kukaa chini na kusaidiana na Serikali kwa ujumla kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi, ili tutoke hapo na kusonga mbele,”

 “Mpina anapaswa atambue kwamba katika kuongoza nchi iko busara inahitajika zaidi, si kila jambo linalotokea ndani ya Serikali lazima lisemwe hadharani, Serikali haiko hivyo, mbona kipindi chao akiwa Waziri walichoma mamilioni ya vifaranga vya kuku vilivyotokea Kenya, Je hiyo ilikuwa busara? Ni bora vingerudishwa vilikotoka,” alieleza. 


Katika hatua nyingine Mgeja ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuchapa kazi na wasipoteze muda kushabika mambo ambayo hayana tija kwa Taifa ambayo huwa na mlengo wa kisiasa zaidi, na kwamba anavyoelewa yeye  kwenye sakata hili la sukari hakuna fedha taslimu ambazo zimeibwa ndani ya Serikali. 


Alisema wizara hizi haziongozwi na malaika, hivyo yapo makosa madogo madogo ya kiutendaji ambayo yanaweza kujitokeza na hata huko nyuma watanzania waliona yapo mambo yalifanyika bila kufuata utaratibu lakini watu walikaa kimya na hata ripoti ya upotevu wa shilingi bilioni 1.5 watu hawakuvalia njuga kama hili la sukari.

 “Tatizo letu ni viongozi wetu kutokupenda kushirikiana na kuwa kitu kimoja, shida yetu ni umasikini wa mawazo, wavivu wa kufikiri lakini pia nafsi zetu zina roho mbaya, roho za chuki, hatuna upendo miongoni mwetu, tuna siasa za kuviziana, hili linaturudisha nyuma kama Taifa,” 


“Ushauri wangu tuvipige vita vitendo hivi ambavyo vinaturudisha nyuma kama Taifa, tulete mapinduzi ya fikra, tukileta mapinduzi ya fikra Tanzania kwenye neema itasonga mbele, maendeleo na maisha bora kwa kila mtanzania itawezekana,” alieleza Mgeja. 

Aliendelea kueleza kuwa moja ya wizara ambazo huko nyuma zilikuwa zikiyumba ni wizara ya kilimo ambayo tangu alipokabidhiwa waziri Hussein Bashe kidogo wizara hiyo imeanza kuonesha mafanikio makubwa ikiwemo kuweka mipango mikakati ya kuwasaidia wakulima husasan vijana wa kitanzania.


 “Kuanzia Serikali ya awamu ya tatu malumbano yalikuwepo hasa kwenye wizara hii ya kilimo upande wa sakata la uhaba wa sukari, hivyo binafsi nashauri tukiwa na uzalishaji mkubwa wa sukari haya malumbano ya kila mara hayatatokea tena,” 


“Malumbano haya mara nyingi yamekuwa yakitumiwa na wanasiasa kama mtaji wa kisiasa, na wengine kutaka kutoana kafara kwa watendaji na viongozi walioko ndani ya wizara, sasa hili lifike wakati liishe, na tutafanikiwa tu kwa kuongeza uzalishaji wa kutosha wa sukari hapa nchini, nakumaliza changamoto za kila mara,” alisema. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com