Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga akimpa pole mama wa mtoto aliyepotelewa na mtoto wake
Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga akizungumza na wananchi baada ya kufika eneo alikoibiwa mtoto mwenye ualbino
Na Mariam Kagenda _Kagera
Watu ambao bado hawajafahamika wamemuiba mtoto mwenye ualbino mwenye umri wa miaka miwili na nusu katika Kijiji cha Bulamula Kata ya Kamachumu Wilayani Muleba mkoani Kagera kisha kutokomea naye kusikojulikana.
Mama wa mtoto huyo ambaye ni Judith Richard amesema kuwa tukio la kuibiwa kwa mtoto wake wa kike aitwaye Noela Asimwe Novath
limetokea nyumbani kwake Mei 30 mwaka 2024 majira ya saa moja jioni na mtoto huyo ni
Bi. Richard amesema kuwa walikuwa wanaume wawili ambapo mmoja alikuja kuomba msaada wa chumvi na baada ya kutoka nje alikabwa na watu hao kisha wakamchukua mtoto wake na kukimbia naye hivyo ameomba Serikali kumsaidia kumtafuta mtoto wake ili aweze kupatikana .
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kamachumu Bwana Leodigad Chonde amesema kuwa tayari wameanzisha ulinzi shirikishi kwa kushirikiana na Jeshi la polisi wa kumtafuta kila sehemu ya Kata hiyo lengo ni kuhakikisha mtoto huyo anapatikana akiwa salama .
Katibu wa chama cha watu wenye ualbino Wilaya ya Muleba Bw. Mahamudu Musedemi ameomba Serikali wilayani Muleba kuhakikisha wanamtafuta mtoto huyo kwani kitendo hicho kinawafanya kuishi kwa hofu.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga amesema Serikali ipo inaendelea na zoezi la kuhakikisha mtoto huyo anapatikana akiwa hai na kuwaomba Wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi la Polisi ili mtoto huyo aweze kupatikana.
Aidha amesema kuwa kitendo hicho sio kizuri na kinatakiwa kukemewa na kila mtu na kuwaomba kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anashiriki kutafutwa kwa mtoto huyo.
Social Plugin