HELPAGE YAMETOA MAFUNZO KWA WANAUME KISHAPU KUACHANA NA TABIA HASI ZITOKANAZO NA MILA NA DESTURI NA KUSABABISHA VITENDO VYA UKATILI




Na Sumai Salum, KISHAPU

Baadhi ya wanaume kutoka Kata Saba Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga,wamepewa elimu ya kutokomeza tabia hasi zitokanazo na Mila na Desturi ambazo husababisha ukatili dhidi ya wanawake,wasichana na watu wenye ulemavu.
 Mkuu wa Program Helpage Tanzania Bw.Leonard Ndamgoba akizungumza kwenye warsha ya siku moja iliyofanyika leo juni 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta Wilayani humo amesema kuwa katika kuendelea kutekeleza mradi wa "Chaguo langu haki yangu" wanaume wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko ya kweli ya kutokomeza masuala ya ukatili.

"Hadi sasa matukio mengi yanaonesha kuwa wanaume ndio chanzo, lakini mbali hayo ni kundi lililokuwa limesahaulika kupewa elimu juu ya masuala ya ukatili lakini sasa Helpage kwa kushirikiana na WAEDO kwa ufadhili wa UNFPA tumeamua kujitoa kuja kwenu kutoa elimu na kusaidiana nanyi wanaume mkiwa ni kiungo kikubwa kwa familia hivyo pia tuongeze ushiriki katika uboreshaji wa afya ya uzazi" amesema Ndamgoba.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Kishapu Bi. Mwajuma Abeid amezungumzia changamoto zitokanazo na Migogoro ya Ndoa na namna inavyoathiri familia kwa kutoa mifano kadhaa ya matukio ya ubakaji na ulawiti huku akibainisha kuwa migogoro mingi chanzo chake ni wanaume na hasa kipindi cha mavuno.

"Takwimu ya robo ya kwanza ya mwezi Januari hadi Machi tumepokea kesi 94 za ukatili wa kimwili wanawake 64 wanaume 30,ukatili wa kihisia wanawake 171 wanaume 82,ukatili wa kingono (ubakaji na ulawiti) wanawake 198 na ulawiti kwa wanaume kesi 8 na hata Juni 11 tunasikiliza kesi mahakamani ya baba kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa darasa la tano(5)", amesema Bi Mwajuma
Mratibu msaidizi wa afya ya uzazi na mtoto halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bi. Rehema Jumanne akielezea madhara ya mimba za utotoni amesema kuwa kutokana na via vya uzazi kutokomaa hupelekea mimba kuharibika,kuzaa mtoto njiti, kutokana na uzazi pingamizi upata Fistula pamoja na vifo.

"Wanaume ni muhimili mkubwa wa familia na waleta mabadiliko kwa jamii hakikisheni mnatenga bajeti ya kununua taulo za kike, kuwapa mahitaji yao na kuzungumza nao uhalisia uliopo ili waweze kuwa na ufahamu wa kufanya maamuzi sahihi pindi wanapofuatwa wanaume waharibifu" ,ameongeza Jumanne.
Warsha hiyo imejumuisha baadhi ya wazee na vijana wa kiume kutoka kata za Mwamalasa,Talaga,Lagana,Mwamashele,Idukilo,Ukenyenge,Mwaweja, watendaji wa vijiji na kata,afisa ustawi wa halmashauri,Afsa maendeleo ya jamii pamoja na mratibu wa Afya ya Uzazi na mtoto huku mradi huo wa "Chaguo langu haki yangu" wenye mwaka mmoja sasa ukiwa na matokeo chanya hadi sasa kutokana na wanaume kuwa na utayari wa kutokomeza tabia za mila na desturi hasi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post