Katibu Mkuu wa kanisa la TLC Dk. Salvatory Mlaga akizungumza na waumini (hawapo pichani) Mara baada ya ibada ya kuombea jamii juu ya matendo maovu iliyofanyika katika kanisa hilo mjini Morogoro
Mwakilishi wa kanisa la TLC Archbishop Prophet Mpala (kushoto) akimpongeza Katibu wa Kanisa hilo Mara baada ya kumaliza ibada ya Jumapili kanisani hapo.
Mwakilishi wa kanisa la TLC Archbishop Prophet Mpala (kushoto) akiteta Jambo na Katibu Mkuu wa kanisa hilo Dk. Salvatory Mlaga Mara baada ya kukamilika kwa ibada ya Jumapili.
(Picha zote na Christina Cosmas, Morogoro)
Na Christina Cosmas, Morogoro
WITO umetolewa kwa madhehebu ya dini kuweka mpango mkakati wa kiroho na kuiokoa jamii ikiwemo watoto kuondokana na tabia za ubakaji, ulawiti na viburi zinazotokana na muingiliano wa kizazi cha tano cha mashetani.
Mwakilishi wa kanisa linalotoa huduma kwa kuzunguka kila mahali duniani (TLC) Archbishop Prophet Mpala alisema hayo Jana aliwataka kwenye huduma ya kuelimisha vijana katika kituo kilichopo kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro.
Archbishop Mpala alisema kwa mujibu wa maandiko ya biblia kizazi cha tano kimemezwa na wanefili au mashetani na hivyo kuzaa kwa asilimia 100 mashetani na asilimia 100 wanadamu ambao ndani yao kuna uadui mkubwa na kuvunja mioyo ya mapendo iliyopandikizwa na Mungu kwa mwanadamu.
Alisema matendo hayo maovu yameanza muda mrefu na kuongezeka mwezi Januari mwaka 2023 na kuharibu kizazi cha tano cha wana wa Misri ambacho kinapaswa kuangamizwa mapema ili kuepusha uharibifu mkubwa wa dunia.
Hivyo aliwashauri viongozi wa dini kuwa na kauli mbiu ya toba na matengenezo ya kizazi hicho na kupata kizazi kipya.
Aidha aliwataka viongozi wa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi mbalimbali kutoa ushirikiano kwa kanisa hilo katika kupatikana vitendea kazi ikiwemo fedha ili kurahisisha mpango kazi kwa kusudi la Mungu.
Naye Katibu Mkuu wa kanisa la TLC Dk. Salvatory Mlaga alitoa wito kwa watoto kujenga tabia ya kufuata mafundisho mema ya wazazi na kanisa kupitia Imani yao kwa Mungu na kuyaacha ya dunia na kama wakibanwa na makundi na wakihitaji kutoka wakimbilie kwa Yesu kupata huduma za kiroho.
Dk. Mlaga alisema katika kueneza nuru ya Kristo kwa kutumia kanisa linalotembea tayari wameshatembelea mikoa ya Tanga, Same -Moshi, Zanzibar na Ifakara, Moro mjini mkoani Morogoro.