Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kahama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza wakati wa mkutano huo
Na Mwandishi Wetu - Malunde 1 blog
Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, umeelekezwa kuzichukulia hatua Taasisi za serikali, viongozi pamoja na wananchi wanaodaiwa ankara za maji hali inayorudisha nyuma juhudi za serikali za kumtua mama ndoo kichwani.
Maelekezo hayo yametolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kahama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro leo Juni 25, 2024 wakati wa mkutano wa mwaka wa wadau wa sekta ya maji wilayani Kahama.
"Kuna viongozi na halmashauri hazilipi ankara za maji nimeshaelekeza wale wadaiwa sugu orodhesheni majina mlete tunajua namna ya kushugulika nayo kama ni mkurugenzi aitwe kwa maana wanaitia aibu serikali, kwenye eneo la ulipaji wa ankara za maji tusiangalie sura",amesema Mtatiro
Awali akisoma taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji na utekelezaji wa miradi ya maji, katika wilaya ya Kahama, Kaimu meneja RUWASA wilaya ya Kahama Mhandisi Paschal Mnyeti amesema jumla ya watu 236, 308 kati ya watu 390,593 waliopo katika halmashauri hiyo, sawa na asilimia 60.5 katika Halmashauri ya Ushetu wanapata huduma ya maji safi na salama, ambapo asilimia 47.3 wanapata huduma ya maji kupitia mtandao wa bomba uliojengwa katika maeneo husika na asilimia 13.2 wanapata huduma ya maji kupitia visimavya pampu za mkono zilizopo katika maeneo husika. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Katika halmashauri ya Msalala taarifa hiyo inaeleza kuwa kwa mujibu wa sensa 2022, halmashauri ya Msalala ina jumla ya wakazi 378, 214, ambapo kati ya hao jumla ya watu 272,314 sawa na asilimia 72 wanapata huduma ya maji safi na salama, ambapo asilimia 64.5 wanapata huduma ya maji kupitia mtandao wa bomba uliojengwa katika maeneo husika, na asilimia 7.2 wanapata huduma ya maji kupitia visima vya pampu za mkono vilivyopo katika maeneo husika.
"Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024, wakala huo umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji yenye mtandao wa mabomba ya kusambaza maji yenye thamani ya shilingi 9,404,453,283.93 yenye uwezo wa takribani watu 62,824 ikiwemo: Upanuzi wa mradi wa maji Kagongwa, ujenzi wa mradi wa maji katika vijiji vya Mwazimba, Mwaningi pamoja na ukarabati wa mradi wa maji katika kijiji cha Bulige uliopo katika halmashauri ya Msalala, upanuzi wa mradi wa Mwakuhenga kwenda vijiji vya Mwankima na Igundu halmashauri ya Msalala",amesema.
Miradi mingine ni mradi wa maji vijiji vya Chona, Ubagwe na Bukomela Halmashauri ya Ushetu, pamoja na Upanuzi wa mradi wa maji Nyankende kwenda kijiji cha Mwadui katika Halmashauri ya Ushetu.
Mbali na mafanikio hayo Mhandisi Mnyeti ameeleza kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti kutokana na kuwepo kwa maeneo mengi yenye uhitaji wa kujengewa miundombinu ya usambazaji maji, matumizi madogo ya maji safi na salama katika maeneo mengi ya vijijini, hususani wakati wa masika hivyo kuathiri dhana nzima ya serikali ya kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama licha ya kutumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji.
Changamoto nyingine ni baadhi ya taasisi kama vile shule za msingi, sekondari zahanati na vituo vya Afya kutolipa ankara zao za maji kwa wakati, na kusababisha baadhi ya vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii kusuasua katika uendeshaji wake.
Kaimu meneja RUWASA wilaya ya Kahama Mhandisi Paschal Mnyeti
Social Plugin