Afisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini Kahama Mhandisi Joseph Kumbulu akizungumza na waandishi wa habari namna walivyoweka mtego na kumkamata tapeli wa madini ya dhahabu aliyekuwa akijitambulisha kuwa yeye ni afisa madini
NA NEEMA ISRAEL- KAHAMA
Wakazi wa Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga wameshauriwa kutokununua madini mtaani bali waende wakauziane na wateja wao kwenye soko la madini ili kuepuka utapeli wa madini ya dhahabu ulioanza kushamiri katika mkoa wa kimadini Kahama.
Wito huo umetolewa Juni 28, 2024 na Afisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini Kahama Mhandisi Joseph Kumbulu baada ya ofisi yake kuweka mtego uliofanikisha kumkamata Mzee AmosiPaulo Mangube mkazi wa Geita aliyekuwa akifanya vitendo vya kuwatapeli wananchi wilayani Kahama huku akijitambulisha kama Afisa madini.
Kwa mujibu wa Kumburu, mzee Mangube amekuwa akifanya vitendi hivyo kwa kusaga kufuli la kufungia mageti na milango na kisha kuiweka kwenye vifungashio maalum huku akidanganya kuwa ni dhahabu.
“Kwa muda wa miezi miwili sasa katika Mkoa wa kimadini Kahama kumetokea wimbi la utapeli kwa baadhi ya watu kujiita maafisa madini wamekuwa wakitumia makufuli yenye rangi ya dhahabu wanayapondaponda na kuweka kwenye chupa wanatapeli watu, kuna watu walikuja kulalamika kuna watu wamewatapeli ambao wanajiita maafisa madini hivyo tulifanya mtego na tukamkamata”,amesema Kumbulu .
Amos Paul mwenye (58) ameeleza jinsi alivyokutwa na madini hayo feki ya dhahabu katika kituo kidogo cha mabasi kilichopo Majengo Kahama, na alipigwa sana na watu wanaojiita polisi jamii manusura kufa ambapo analishukuru jeshi la polisi kufika katika eneo hilo na kumuokoa kwa watu wenye hasira kali akiwa hoi.
Amos ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Madini , mkoa wa kimadini Kahama kwa kumsamehe baada ya kukiri makosa yake na kumpa elimu, pia amewatahadharisha wananchi wenye tabia ya utapeli waache maana utapeli ni kifo.
Alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo, kaimu kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Kennedy Mgani alisema kuwa bado halijafika mezani kwake na kuahidi kuwa analifuatilia na kwamba atalitolea ufafanuzi baadae litakapokamilika.
Mzee Amos Paulo Mangube mkazi wa Geita aliyekuwa akifanya vitendo vya kuwatapeli wananchi wilayani Kahama huku akijitambulisha kama Afisa madini
Vipande vya kufuli vilivyo pondwapondwa vinanyotumika kutapeli watu kwamba ni madini ya dhahabu