Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAVUVI HARAMU ZAIDI YA 200 WAKAMATWA WAKITUMIA NYAVU HARAMU NA MABOMU

Na Hadija Bagasha Tanga, 


WAVUVI haramu zaidi ya 200 wamekamatwa katika vijiji vilivyopo kando ya mwambao wa bahari ya Hindi, wilayani Mkinga wakituhumiwa kutumia nyavu zisizo rasmi pamoja na mabomu na kuua mazalia ya samaki na viumbe wengine wa majini.

Katibu wa Shirika linalojihusisha na utunzaji na usimamiaji wa rasilimali za bahari  katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi, Ahmed Salim Omari amebainisha hayo kwenye hafla ya kukabidhi boti ya doria yenye thamani ya shilingi milioni 30 wilayani humo. 

Omari amekabidhi boti hiyo kwenye kamati ya usimamizi wa maendeleo ya pamoja ndani ya vijiji vilivyopo mwambao wa bahari ya Hindi katika wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga.

"Sisi Mwambao tunashirikiana na serikali katika uhifadhi wa rasilimali za bahari na pwani, na kauli mbiu yetu kuu ni kwamba, Afya ya bahari ndiyo uchumi wa Jamii' tukiamini kwamba kama bahari itaboreka na yale mazalia ya samaki yataendelea kuimarika samakii watakuwa wengi,

"Na vile vile jamii itanufaika na samaki hao na hiyo ndio dhana yetu na tunapigana nayo kuhakikisha kwamba tunanyanyua uchumi wa watu katika ukanda wa bahari.

Ameeleza kwamba katika kupambana na kuhakikisha wanafikia hatua hiyo wanayo mikakati miwili ambayo ni kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ili wananchi waachane na uvuvi haramu, kwani wakiwa wameelimika na kuachana na uvuvi huo samaki wataendelea kukua na uchumi wao utaimarika.

Lakini vilevile amesema wananchi ambao wanakuwa ni wagumu kuelewa elimu hiyo, wanafanya msako na kutoa boti ambazo zinakwenda kwenye kina wanakovulia na kuwakamata lakini pia kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya sheria.

"Na boti hizi tunazokabidhi hapa zilishaanza kufanya msako kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita na tumeweza kuwakamata wavuvi haramu 203 ambao wamepelekwa kwenye vyombo vya Sheria,

"Miongoni mwa hatua ambazo zimechukuliwa ni kuwatoza faini ya sh milioni 5.3 na ambazo zimeingizwa katika halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kama mapato, kwahiyo tunaona ni namna gani Shirika la Mwambao halisaidii wananchi tuu bali hata halmashauri tuna kazi nayo" amesema.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkinga, Palango Abdul kwa niaba ya mkuu wa Wilaya hiyo, ameagiza kuendelea kuchukuliwa kwa hatua stahiki kwa wavuvi wanaokamatwa ili kukomesha uvuvi haramu katika Wilaya hiyo.

Kwa upande wake katibu wa kamati ya utunzaji wa mazingira ya bahari  kijiji cha Mwaboza, Salimu Kibao amesema tangu wameanza kutunza mazingira ya bahari uvuaji wa samakii aina ya pweza meongezeka kutoka kilo nne hadi kufikia tani tatu za samaki hao.

Boti  hiyo ya  zaidi ya sh milioni 30 ni ya pili kutolewa na shirika hilo, kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali za kutunza mazingira ya bahari na kuilinda raslimali bahari ili iweze kunufaisha kizazi cha sasa na kizazi kijacho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com