Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC KILAKALA ATAKA WATUMISHI WA AFYA KUTANGULIZA UTU BADALA YA FEDHA KWANZA

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala
Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala

Na Hadija Bagasha Tanga

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala amewataka watumishi wa afya wilayani humo kutanguliza utu badala ya kutanguliza maslahi ya fedha mbele ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa sambamba na kuwaasa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa weledi.

Mkuu huyo ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga.

Kilakala amefafanua kwamba wapo wananchi wengine wanakwenda kutibiwa wakiwa wameshikika na ugonjwa, hivyo kumuuliza fedha badala ya kumtibia yanaweza kutokea madhara makubwa yatakayopelekea baadaye watu kuanza kunyoosheana vidole.


"Mtu amekuja na mnamuona anahitaji kutibiwa kwa haraka kwanza kabla ya fedha msisubirie msaidieni, madaktari na wauguzi mara kadhaa nimewaelekeza, watibieni hawa wananchi ili wasipoteze maisha, mimi mkuu wenu nipo tutasaidiana,

"Tusipoteze wananchi wetu, eti kwasababu ya fedha, yale mambo yaliyotokea katika Wilaya zingine na Mikoa mingine katika huduma za afya, tunajipanga ili Wilaya yetu ya Pangani, tunaendelea kujipanga zaidi yasiendelee kutokea", amesema.

Kilakala ameendelea kusisitiza watumishi hao kutoa kipaumbele kwa wakina mama wajawazito, wakina mama wenye watoto wachanga pamoja na wazee, ambapo kadi zao zinapaswa kutumika, ili wapatiwe matibabu.

Sambamba na hilo, mkuu huyo amesema wamejipanga kuongeza mapato ya halmashauri ya Wilaya hiyo kwakuwa bado ukusanyaji wake ni mdogo sana hivyo wamechukua jitihahada za makusudi katika kipindi cha kuelekea miezi sita kuhakikisha wanakusanya zaidi.

"Na sisi watu wa Pangani tumeamua kumuunga mkono Rais wetu kutoka kwenye nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi, na hili ni azimio kutoka mwaka 2024 hadi 2034, kwa Mkoa wa Tanga, Wilaya hii imeona fursa ya kwenda kuwekeza katika hewa ya ukaa,

"Ili Halmashauri yetu upate mapato mengi, tutahakikisha tunapungiza wimbi la ukataji wa miti hovyo katika maeneo yetu, tukishakuwa na biashara ya hewa ya ukaa vijiji vitajitegemea na kuwa na miradi mikubwa ya maendeleo", amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com