NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KARIBU asilimia 80% ya shughuli za kibinadamu zinasababisha mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo Jamii imetakiwa kuhakikisha inatunza mazingira kwa kupanda miti na kuacha kukata miti hovyo pamoja na kutunza vyanzo vya maji ili kupunguza mabadiliko ya tabianchi ambayo inaonekana kumuathiri kwa kiasi kikubwa mwanamke.
Hayo yamebainishwa leo Juni 5, 2024 Jijini Dar es Salaam katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambazo hufanyika kila Jumatano katika viwanja vya TGNP- Mtandao, Mabibo.
Wamesema sababu zinazopelekea athari ya uharibifu wa ardhi, ukame na jangwa kwa wanawake na makundi yaliyopo pembezoni ni pamoja ukosefu wa maji ambapo itamlazimu kwenda mbali kutafuta maji bila mafanikio na muda mwingine inamsababishia hata kuweza kubakwa.
Pia sababu nyingine ambayo inaweza kumuathiri mwanamke ni pamoja na gharama kubwa za mbegu pamoja na mbolea kwaajili ya kilimo cha kisasa ambacho kitaweza kumsaidia kumudu kutokana uharibifu wa ardhi, ukame pamoja na jangwa.
Kwa upande wake, Mdau wa Jinsia na Maendeleo, Hans Obote amesema kutokana na maeneo mengi ya mjini wanawake wamekuwa wakijipatia kipato kupitia shughuli za kilimo kidogo (bustani) hivyo kutokana uharibifu wa maeneo ya kulima hasa ardhi inapelekea mwanamke huyo kukosa maeneo mengine ya kufanya shughuli hizo na kumfanya asiendelee na shughuli hiyo.
Zainabu Mzaray ambaye pia ni Mdau wa Jinsia na Maendeleo amesema ukosefu wa maji kwa mwanamke inampelekea kukosa kujiamini pindi akiwa kwenye hedhi ambapo shughuli zote ambazo alikuwa anazifanya zinasimama.