KLINIKI YA KISHERIA YAZINDULIWA DODOMA


Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amezindua Kliniki ya Ushauri na elimu ya Sheria kwa Umma inayokusudia kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi ili kupunguza migogoro dhidi ya Serikali na kupata suluhu ya changamoto. 

Kliniki hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili wa Serikali ni agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka viongozi kuwa na utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaongoza katika taratibu za kupata haki. 

Akizindua Kliniki hiyo leo June 26,2024 Jijini Dodoma, Dkt. Feleshi amesema Kliniki hiyo itaimarisha utawala wa Sheria nchini ikiwa ni pamoja na kuchochea mazingira ya amani kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi. 

"Kipekee natoa rai kwa Mawakili wote wa Serikali hapa nchini kutenga muda na kusikiliza wananchi kupitia maeneo yao, niwakumbushe pia wakuu wa mikoa na Wilaya ambao bado hawajakamilisha kuteua wajumbe wawili wa kamati za ushauri wafanye hivyo ili kamati hizo zianze kusikiliza malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa, "amesema

Kipekee, Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali amevikumbusha vyama vya Mawakili wa Serikali (TPBA)pamoja na Mawakili wa Tanganyika (TLS)kuendelea kushirikiana na Serikali na kamati za ushauri wa kisheria ngazi za mikoa na Wilaya ili kusikiliza malalamiko na kuyatatua kwa wakati. 

Amesema Kliniki zitakazo endeshwa na Kamati hizo zitakuwa endelevu kwa nchi nzima na hivyo kuwataka wananchi wa Dodoma na Mikoa jirani kupata huduma ya Ushauri wa kisheria bure kuanzia June 26 hadi Julai 3,2024 kuanzia saa 2.00 asuhubi hadi saa 10.00 jioni.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo ameeleza kuwa wananchi wakiendelea kutatuliwa kero zao uzalishaji utakua kwa kasi. 

Amesema Serikali kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia wananchi wamekuwa sehemu ya mabadiliko kwa kuelewa namna ya kutafuta suluhu ya malalamiko yao. 

"Kezo za wananchi ni wajibu wetu, tuendelee kuwa pamoja katika kuzitatua kupitia ushirikiano wetu, kupitia hizi siku zilizoyengwa wananchi wataendelea kuzitumia vizuri kuelimishwa zaidi ili wapate haki yao na kuwa na amani, " amesema

Amesema wataendelea kuboresha mifumo ya msaada wa kisheria kupitia digitali na simu za kawaida ili kufanikisha huduma bora kwa wananchi. 





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post