MADETE ANG’OLEWA UENYEKITI UVCCM SHINYANGA MJINI


Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog

Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga CCM imemuachisha nafasi ya uongozi aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho wilaya ya Shinyanga Mjini Ndg. Jonathan Agustino Madete kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia kikao kilichoketi leo Juni 13, 2024 katika jengo la ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga.

Akisoma maamuzi yaliyofikiwa na kikao hicho wakati akizungumza na vyombo vya habari Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga CCM Ndg. Richard Raphael Masele amesema kikao cha halmahsauri kuu ya CCM Mkoa wa Shinyanga Mjini chini ya mwenyekiti wake Ndg. Mabala Mlolwa kimemuachisha nafasi ya uongozi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wilaya ya Shinyanga Mjini na kuazimia kutofumbia macho wala kumvumilia yeyote atakayevunja kanuni na katiba ya chama hicho.

“Kikao cha Halmashauri kuu ya CCM, Mkoa wa Shinyanga chini ya Mwenyekiti wake Ndg. Mabala Mlolwa kilichoketi mnamo 13.06.2024 pamoja na mambo mengine kimemuachisha nafasi ya uongozi Ndg. Jonathan Agustino Madete aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga Mjini kwa sababu za utovu wa nidhamu”, amesema Richard Masele.

“Vile vile halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Shinyanga kamwe haitamfumbia macho wala kumvumilia mtu yeyote kiongozi au mwanachama atakayevunja kanuni, taratibu na katiba ya chama chetu, hatua za kinidhamu zitachukuliwa mara moja, hii ni pamoja na kulinda heshima ya chama chetu na jumuiya zake”, ameongeza Richard Masele.

Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga CCM Ndg. Richard Raphael Masele akizungumza na vyombo vya habari.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga Mjini Ndg. Jonathan Agustino Madete.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post