Uongozi wa IAA kupitia idara ya usimamizi wa biashara umeandaa maonesho ya ujasiriamali (Grand Entrepreneurship & Innovation Exhibition) yanayofanyika chuoni hapa na kushirikisha wanafunzi kuonesha ujuzi, na vipaji walivyonavyo pamoja na maandiko yao ya biashara.
Akimwakilisha Mkuu wa Chuo katika Maonesho hayo Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Epaphra Manamba amesema uongozi wa Chuo umekuwa ukiandaa Maonesho haya katika kutekeleza sera ya elimu ya Taifa, jambo ambalo limepelekea kuwapa wanafunzi ujuzi na maarifa ya kupambana na soko la ajira wanapomaliza masomo yao.
Prof Manamba ameongeza kuwa kama Chuo wanahakikisha kuwa wanafunzi wanafikia malengo ambayo Chuo, wazazi na wanafaunzi wenyewe wamejiwekea, hivyo kupitia Maonesho haya wanathibitisha jambo hilo kutokana na vitu vinavyooneshwa na wanafunzi wao kwa vitendo.
“Kama mwanafunzi hakikisha ubunifu uwe ndio kitu cha kuzingatia ukiwa chuoni, na ili uwe na wazo zuri katika ujasiriamali ni lazima uangalie wapi kuna mapungufu kwenye soko ili uje na kitu kimpya” amesema Prof. Manamba
Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo cha Usimamizi wa Biashara na Manunuzi IAA, Dkt. Grace Idinga amewataka wanafunzi kuhakikisha chochote walichokipata kupitia masomo yao na Maonesho hayo, wahakikishe wanakifanyia kazi kwani mtaani nafasi hii inapatikana kwa gharama
Naye Afisa Biashara wa Jiji la Arusha Bw. Dominick William amewaasa wanafunzi kuwa ni vyema wakaendelea kuwa wabunifu, kuwa na uvumilivu kupenda wanachokifanya na kuwa wenye kujifunza kila siku ili kuongeza thamani na kukomaa Zaidi katika sekta ya ujasiriamali.
Maonesho haya yanatarajiwa kufanyika kwa takribani siku nne kuanzia tarehe 18 mpaka 21 mwaka 2024.
Social Plugin