MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameihoji serikali ni lini kituo cha afya cha Ntuntu kilichopo jimboni kwake kitaanza kufanya kazi.
Mtaturu ameuliza swali hilo Juni 10,2024,Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu.
"Mh Mwenyekiti,kituo cha afya cha Ntuntu kilitengewa Sh Milioni 500 huu unaenda mwaka wa pili lakini hakijaanza kufanya kazi pamoja na kwamba tulipata fedha kwa awamu tofauti,
"Nataka nijue ni lini kituo hicho kitaanza kufanya kazi kwa sababu wananchi wanakisubiri kwa muda mrefu na ni kituo cha mkakati,".amehoji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),Dkt.Festo Dugange amekiri kuwa ni kweli kuna baadhi ya vituo vya afya ambavyo vilijengwa na kukamilika lakini bado havijaanza kutoa huduma.
"Naomba niwakumbushe na kuwasisitiza wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kikiwemo na kituo cha afya cha Ntuntu, baada ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha na kukamilika kwa vituo,matarajio ya wananchi ni kuanza kupata huduma kupitia vituo hivyo,
"Serikali haitakuwa tayari kuona kituo kimekamilika lakini hakitoi huduma na wananchi wanahitaji huduma,naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi kuhakikisha ndani ya miezi miwili kituo hicho kianze kufanya kazi na wananchi wapate huduma,".ameelekeza.
Social Plugin