Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeshiriki mkutano mkuu wa 65 wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE). Mkutano huo ulifunguliwa tarehe 20 Juni 2024 na Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye alimuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Katambi amesema ni maagizo na maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa taasisi zote za Serikali kushirikiana na taasisi za binafsi katika usimamizi mzuri wa sera, sheria, taratibu, kanuni, mipango na mikakati ya Serikali ili kufikia malengo ya pamoja.
Naye, Meneja Uandikishaji, Ukaguzi na Matekelezo wa NSSF, Cosmas Sasi amesema Mfuko unaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi yakiwemo kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Amesema hivi sasa NSSF imetoa msamaha kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango na tozo itokanayo na ucheleweshaji wa michango.
Bw. Sasi amesema kuwa Bodi ya Wadhamini ya NSSF imetoa msamaha wa tozo kwa waajiri wote wa sekta binafsi. Amebainisha kuwa katika msamaha huo waajiri wote ambao wana malimbikizo ya michango watakaolipa malimbikizo yao yote hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2024 watapata msamaha wa tozo kwa asilimia 100.
Kwa waajiri ambao watalipa malimbikizo yote kati ya tarehe 1 Agosti, 2024 hadi 31 Agosti, 2024 watapata msamaha wa tozo kwa asilimia sabini na tano (75) na waajiri wote ambao hawana malimbikizo yoyote ya michango ya wanachama wanayodaiwa na NSSF mpaka kufikia tarehe 31 Mei, 2024 na kuendelea hadi tarehe 31 Julai, 2024 watasamehewa tozo zote wanazodaiwa kwa asilimia mia moja 100.
Bw. Sasi amesema NSSF imepiga hatua kubwa kwenye TEHAMA ambapo waajiri wanaweza kujisajili na kusajili wafanyakazi wao na kuwasilisha michango bila kufika katika ofisi za NSSF kupitia mfumo wa huduma binafsi kwa mwajiri (Employer portal).
“Maendeleo haya ya TEHAMA yamesaidia katika kuongeza ufanisi na kukuza thamani ya NSSF pamoja na kuongeza wanachama," amesema Bw. Sasi.