Na Mathias Canal, Kagera
Wakala wa Barabara “TANROADS” Mkoani Kagera inasimamia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 1,966.29. Kati ya hizo barabara kuu ni Kilomita 861.59, barabara za mkoa ni kilomita 1,053.75 na barabara za wilaya ni kilomita 50.95.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Ntuli John Mwaikokesya mara baada ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja na Uwekaji Taa za barabarani.
Amesema kuwa licha ya kusimamia matengenezo ya barabara na madaraja, katika kipindi cha miaka mitatu Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Kimkakati ambayo utekelezaji wake upo kwenye hatua mbalimbali na jumla ya miradi hiyo inagharimu Tshs bilioni 431.474
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba (Rwamishenye round about) – Bukoba Port Km 5.1 unaojengwa kwa gharama ya Tshs Bilioni 4.641 unaotekelezwa na Mkandarasi mzawa wa kampuni ya M/s Abemulo Contractors Co. ltd ambapo mpaka hivi sasa umefikia asilimia 31.
Mradi mwingine ni Ujenzi wa daraja la kitengule lenye urefu wa mita 140 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 18 kwa gharama ya Tshs Bilioni 31.55 Mradi huo umefikia asilimia 99.0 na unatekelezwa na Mkandarasi M/s China Henan International Cooperation Group CO, LTD (CHICO) ambapo serikali imechangia Tshs. Bilioni 26.55 na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Kagera umechangia TShs. Bilioni 5.00
Mhandisi Mwaikokesya ameongeza kuwa mradi mwingine ni wa Uwekaji wa taa za barabarani katika miji na vitongoji katika Mkoa wa kagera ambapo jumla ya taa 486 za barabarani na taa 4 za kuongozea magari zimewekwa katika miji na vitongoji mbalimbali katika wilaya za mkoa wa Kagera.
“Tumeweka taa 278 za barabarani katika wilaya ya Bukoba na Taa 4 za kuongozea magari, Pia Karagwe-Taa 37, Kyerwa – Taa 44, Ngara- Taa – 66, Biharamulo – Taa 11, na Muleba – Taa 46, Vilevile katika mwaka huu wa fedha 2023/24, jumla ya taa 573 zenye thamani ya Tshs Billioni 2.292 zinatajiwa kufugwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera” Amekaririwa Mhandisi Mwaikokesya
Miradi mingine ni Ujenzi wa barabara inayounganisha Mkoa wa Kagera na Kigoma ya Nyakanazi –Kidahwe; kipande cha Nyakanazi- Kabingo (Km 50) kwa kiwango cha lami ambapo kilomita 30 zipo Mkoa wa kagera na Kilomita 20 zilizosalia zipo Kigoma. Mradi huo unatekelezwa chini ya Mkandarasi mzawa M/s Nyanza Road Works Ltd. Kwa gharama ya Tshs. Bilioni 47.9 na mradi umekamilika kwa asilimia 100 na tayari barabara imeanza kutumika.
Hali kadhalika serikali ya awamu ya sita imeanza Ukarabati wa barabara ya Lusahunga–Rusumo (km 92) kwa kiwango cha lami ikijengwa na Mkandarasi: M/s China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa Gharama ya Tsh Bilioni 153.564. Barabara hii ni moja kati ya mtandao wa barabara muhimu za mkoa wa Kagera ambayo inaunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na DRC kupitia Daraja la Rusumo/Mpakani na Rwanda.
Pia Mhandisi Mwaikokesya amesema kuwa TANROADS Mkoa wa Kagera imeanza Ujenzi wa barabara inayounganisha wilaya ya karagwe na Ngara kupitia hifadhi ya Burigi chato ya Bugene-Kasulo- Kumunazi (Km 128.5), kipande cha Bugene-Burigi Chato (Km 60), Mradi huo unatekelezwa kwa miezi 30 na Mkandarasi wa kampuni ya China Road and Bridge Cooperation ya China (CRBC) kwa gharama ya TSh. Bilioni 92.84 ambapo hadi hivi sasa mradi umefikia asilimia 41.9
“Pia tunaendelea na Ujenzi wa barabara ya kutoka Kagera sugar Juntion (Bunazi) –Kagera Sugar –Kitengule Junction (Km 25); inayotekelezwa na Mkandarasi: M/s China Henan International Cooperation Group CO., LTD (CHICO) kwa gharama ya Bilioni 54.79 kwa muda wa miezi 24” Amesisitiza Mhandisi Mwaikokesya
Kadhalika amesema TANROADS inaendelea na ujenzi wa mradi wa barabara inayounganisha Tanzania na Uganda ya Omurushaka (Chonyonyo) – Nkwenda - Kyerwa (Km 50) kwa kiwango cha lami ikijengwa na Mkandarasi: M/S Shandong Luqiao Group Co Ltd kwa gharama ya Tsh Bilioni 94.093 na kukamilika ndani ya miezi 36.
Social Plugin