RAIS SAMIA AMUAGIZA MSAJILI WA HAZINA KUFUATILIA HESABU ZA MASHIRIKA YOTE KWENYE MFUMO




Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wakati wa hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa Gawio na Michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu Juni 11,2024 Jijini Dar es Salaam.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Msajili wa Hazina, Thobias Makoba, akizungumza wakati wa hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam. Na: Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu kuhakikisha anaweza kuona hesabu za mashirika yote anayoyasimamia ikiwa ni pamoja na makusanyo na matumizi yao.

Rais Samia ameyasema hayo katika hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Mashirika na Taasisi za Umma, iliyofanyika Juni 11, 2024 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kuona kile kinachoingia na kinachotoka kwani hiyo itasaidia kufahamu uwezo wa mashirika hayo kiuchumi na namna yatakavyoweza kujisimamia yenyewe.

"Yapo mashirika ambayo yanaweza kabisa kusimama yenyewe, mfano Ngorongoro inaweza kusimama yenyewe kwa sababu tumetengeneza mazingira watalii wanakuja mpaka wanacheua sasa kwanini isisimame, kwanini Tanapa isisimame yaani hakuna sababu.

“Naziagiza bodi za mashirika kubadilika na kuyasimamia kikamilifu hakuna sababu ya mashirika na taasisi zote za Serikali katika kutekeleza hili. Hakuna sababu ya mashirika haya yasiweze kujisimamia yenyewe" amesema Mhe Rais.

Aidha ameongeza kuwa ameridhishwa na uwepo wa ushindani wa wajumbe wa bodi katika kupata nafasi hizo na kwamba hatua hiyo itapelekea kuwapata wajumbe wa bodi wenye weledi na wanaofahamu vizuri mambo yanayoendelea ndani ya mashirika.

"Jambo zuri ni kwamba mjumbe wa bodi sasa watashindana kuitaka nafasi hiyo katika Shirika au Taasisi unayoitaka itabakia nafasi yangu ya mimi kuchagua Mwenyekiti" ameongeza Rais Samia.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema kuwa Ofisi yake ipo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti taarifa za kiutendaji na wakuu wa Taasisi kwa kumwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati kwa mamlaka za uteuzi.

Aidha, amesema Ofisi hiyo imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika vilivyoingizwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina.

"Vigezo hivi vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi, na tutaendelea kuboresha vigezo hivi mara kwa mara, kwa kutegemea mrejesho kutoka taasisi zetu hizi ambao ndio wadau wetu" amesema Mchechu.

Mchechu ameongeza kuwa, pia Ofisi hiyo imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia kwenye sekta nyeti za uchumi.

"Kwenye sekta ya madini kumekuwa na mazungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini. Tumeweza kuongeza hisa za Serikali katika baadhi ya Kampuni, Mathalani tumeongeza hisa za Serikali katika Kampuni ya madini ya Sotta kutoka 16% hadi 20%, jambo litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo" ameongeza Mchechu.

Sambamba na hilo pia wamefanikiwa kukamilisha majadiliano na kuingia mikataba mipya ya wanahisa na kampuni ya NMB, NBC na MCCL, ambapo kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza kupata faida mwaka huu na kutoa gawio kwa wanahisa mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10.

Kuhusu gawio, Mchechu ametoa Rai kwa Mashirika ambayo yanadaiwa kuhakikisha wanakamilisha malipo yao kabla ya mwisho wa Mwaka huu wa fedha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akipokea Gawio la Sh. Bilioni 57.3 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhede (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kulia) wakati wa hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Wakala, Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa, hafla hiyo ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 11, 2024. (Na Mpiga Picha Wetu).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post